2017-07-03 14:06:00

Papa Francisko mgeni rasmi, Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka 2017


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 3 Julai 2017 ameshiriki katika ufunguzi wa Mkutano mkuu wa 40 wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, unaozishirikisha nchi 194 na wajumbe zaidi ya 600. Katika mkutano huu, ametangaza rasmi kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi lililotolewa kwake na Professa Josè Graziano da Silva la kutembelea Makao Makuu ya FAO, tarehe 16 Oktoba 2017 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2017. Siku hii itaongozwa na kauli mbiu “Kubadili mwelekeo wa wahamiaji”.

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wameanza kutafakari kwa kina na mapana changamoto endelevu kuhusu masuala ya usalama wa chakula duniani; athari za mabadiliko ya tabianchi; changamoto katika sekta ya kilimo pamoja na mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Wajumbe wa mkutano wanaendeelea kupembua na hatimaye, kuridhia mpango mkakati wa FAO kwa Mwaka 2018 – 2019. Jumuiya ya Kimataifa inataka kulivalia njuga tatizo la ukame ambalo kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa ni janga kubwa kwa watu wengi Barani Afrika.

Baa la njaa linakuzwa pia kutokana na vita, kinzani, ghasia na migogoro ya kijamii inayoendelea huko: Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini. Jumuiya ya Kimataifa inataka kupambana kikamilifu na baa la njaa duniani, ili hatimaye, kuitokomeza kabisa kwa kuwekeza katika usalama wa chakula sanjari na kuwajengea wakulima wadogo wadogo uwezo. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji nalo ni changamoto kubwa katika kukabiliana na uhakika wa usalama wa chakula na lishe duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.