2017-07-03 10:05:00

Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wanataka amani!


Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume, “Africae munus” yaani “Dhamana ya Afrika” anapenda kuwaalika viongozi wa Kanisa Barani Afrika, kuwa kweli ni wahudumu wa upatanisho, haki na amani; kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, ili kutekeleza kwa dhati kabisa wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwamba, familia ya Mungu Barani Afrika inaitwa kusimama na kusonga mbele kwa imani, matumaini na mapendo. Ili kuweza kutekeleza dhamana hii, viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa watumishi waaminifu, wakweli na wadumifu wa Neno la Mungu.

Kristo katika moyo wa familia ya Mungu Barani Afrika ni chemchemi ya upatanisho, haki na amani. Hii ni dhamana inayowajibisha na kuwahamasisha viongozi wa Kanisa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho Barani Afrika, kwa kutambua kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakuna haki ya kweli isiyofumbatwa katika upendo na amani, changamoto kwa familia ya Mungu Barani Afrika kujipatanisha na Mwenyezi Mungu. Wakristo wawe mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kudumisha haki na upendo, ili amani iweze kutawala katika akili na nyoyo za watu!

Kwa hakika, upatanisho halisi tu ndio unaoweza kuleta amani ya kudumu katika jamii. Hili ni jukumu la wadau mbali mbali ili kweli mchakato wa upatanisho usaidie kuganga na kuponya madonda ya migogoro, kinzani, ghasia na mipasuko ya kijamii, ili kweli umoja, amani, upendo na mshikamano viweze kutawala tena. Kutokana na upatanisho, baada ya vita ya muda mrefu mataifa yanaweza kurudisha amani; majereha ya mauaji ya kimbari yanaweza kuponywa na watu kuanza kupata tena heshima, utu na haki zao msingi. Huu ni mwanzo wa mapambazuko mapya katika mchakato wa maendeleo na amani ya kudumu kati ya watu!

Jamii inapaswa kujisimika katika utamaduni wa kumwilisha haki na amani kwa kuwa na mifumo inayotekeleza dhamana hii kikamilifu! Ikumbukwe kwamba, upendo katika ukweli ni chemchemi ya amani na furaha ya kweli inayomsikwa katika huduma makini kwa jirani! Kutokana na changamoto hii ya Kanisa kuwa kweli ni chombo na mhudumu wa haki, amani na upatanisho, ndiyo maana Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, linaendelea kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika mchakato wa kulinda na kudumisha amani nchini humo kwani wananchi wamechoshwa na mlio wa mtutu wa bunduki! Haiwezekani vita kuendelea kusambaa kila siku kama “moto wa mabua” kwa ajili ya kuwanufaisha watu wacheche wenye uchu wa mali na madaraka!

Mkataba wa amani uliotiwa sahihi hivi karibuni, umehifadhiwa kwenye makabti ya chuma na watu wanaendelea kutwangana kana kwamba, hawana akili nzuri! Watu wasiokuwa na hatia wanaendelea kupoteza maisha! Watu wanalazimika kwa mara nyingine tena kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao! Haiwezekani wananchi wakaendelea kuishi kwa hofu kiasi hiki wanasema Maaskofu wa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Haiwezekani wananchi wa taifa moja, wakaendelea kutwangana kana kwamba, hawafahamiani hata kidogo. Umefika wakati wa kuachana na utamaduni wa kifo na kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, ili amani ya kweli iweze kupatikana nchini humo. Damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumlilia Mwenyezi Mungu wanasema Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Mwenyezi Mungu anawataka watu kutubu na kuongoka, kuacha matendo yao maovu na kuanza kutembea katika njia ya haki, amani, upendo na mshikamano. Ukarimu na upendo ni njia muafaka sana ya kujenga na kudumisha majadiliano na hatimaye, upatanisho wa kweli!

Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, linasema, kuna haja pia ya kujenga na kudumisha utawala wa sheria, ili wale wote wanaohusika katika kuchochea ghasia, vurugu na mauaji wachukuliwe hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani, ili sheria iweze kushika mkondo wake na watu kuanza kujenga imani na matumaini katika mfumo wa utawala bora unaozingatia: sheria, haki msingi, utu na heshima ya binadamu! Kuna haja ya kuambata Injili ya amani ili kuondokana na hofu, chuki, uhasama na tabia ya kutaka kulipizana kisasi. Badala yake, wananchi waheshimiane na kuthaminiana na kwamba, wote wahusishwe katika mchakato wa ujenzi wa nchi yao kwa kuwekeza karama, vipaji na rasilimali mbali mbali walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuvuka kishawishi cha kuvurugwa na kugawanywa kwa misingi ya kiitikadi, kidini na kikabila na badala yake wasimame kidete kulinda, kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa, ili kukuza misingi ya haki, amani, chachu muhimu sana ya maendeleo endelevu ya mwanadamu. Watu wasimamde kidete kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kumezwa mno na ubinafsi, uchoyo, uchu wa mali na madaraka. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kuwaunga mkono, ili kweli misingi ya haki, amani na upatanisho viweze kutawala tena katika akili na nyoyo za watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.