2017-07-03 10:31:00

Kardinali Turkson: Amani ya kudumu! Onesheni utashi wa kisiasa!


Vita, ghasia na vurugu zinazoendelea Sudan ya Kusini ambayo ni kati ya mataifa change zaidi duniani, zinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Vita ya wenyewe kwa wenye inayofumbatwa katika uchu wa mali na madaraka; ukabila na udini usiokuwa na mvuto wala mashiko ni chanzo kikuuu cha mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini yanayoendelea kugumishwa pia na ukame wa kutisha na baa la njaa ambalo linapukutisha maisha ya watu nchini humo. Kumekuwepo na mauaji ya kutisha nchini Sudan ya Kusini, kiasi kwamba, kuna mamilioni ya watu yanayokimbia kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao katika nchi jirani.

Katika shida na mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini, Kanisa limekuwa daima sauti ya wanyonge, chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa wale wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii! Baba Mtakatifu Francisko bado ana matumaini kwamba, iko siku, ataitembelea familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, ili kuitangazia Injili ya amani, upendo, umoja na mshikamano wa kidugu licha ya tofauti zao msingi. Kuna watu wanapambana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kwa watoto wao! Vita imekuwa ni kikwazo kwa watoto wengi kushindwa kwenye shuleni, kiasi kwamba, mustakabali wa watoto hawa kwa siku za usoni, uko mashakani.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini ameamua kuonesha uwepo wake wa karibu kwa kufadhili miradi itakayosaidia kutoa huduma kwa waathirika wa vita, baa la njaa na magonjwa pamoja na kusaidia kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi, ili kuanza kuandika historia mpya ya maisha yao. Mradi huu unajulikana kama “Baba Mtakatifu kwa ajili ya Sudan ya Kusini”. Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, licha ya msaada wa hali na mali uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, lakini bado Vatican kwa kutumia diplomasia yake, inapenda kujielekeza zaidi katika mchakato wa kutafuta amani na maridhiano kati ya wananchi wa Sudan ya Kusini.

Kardinali Turkson kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amekwisha wahi kwenda Sudan mara mbili ili kuonesha mshikamano wa Baba Mtakatifu na Kanisa nchini Sudan ya Kusini pamoja na kuiomba Serikali iweze kuanzisha mchakato wa amani na utulivu kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia: ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Sudan ya Kusini! Hadi sasa Serikali ya Sudan ya Kusini imeonesha nia ya kushirikiana na Kanisa katika kutafuta suluhu ya machafuko ya kisiasa nchini humo.

Msaada uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika masuala ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi ni kidogo sana ikilinganishwa na hali halisi! Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu linaendelea kujipanga, ili kwenda nchini Sudan ya Kusini kujionea hali halisi na hatimaye, kuchukua hatua muafaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wanaoendelea kufariki dunia kutokana na vita, njaa, magonjwa pamoja na wakimbizi wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Hali ya maisha ni tete, wafanyakazi kwa muda mrefu hawapati mshahara, hawawezi kwenda katika shughuli za huduma na uzalishaji na matokeo yake ni ghasia na hali ya kujikatia tamaa!

Kardinali Peter Turkson anakaza kusema, haitoshi kuwa na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na wawakilishi wengine huko Sudan ya Kusini, kama hakuna amani, juhudi zote hizi ni bure! Mwenyeheri Paulo VI anasema, jina jipya la maendeleo endelevu ya binadamu ni amani inayomsikwa katika upendo, haki, umoja na mshikamano. Bila amani, ndoto ya kuleta maendeleo kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini, itabakia kuwa ndoto peke yake! Kumbe, kuna haja ya wanasiasa na wadau mbali mbali nchini humo, kuonesha utashi wa kisiasa kwa kutaka amani iweze tena kutawala nchini Sudan ya Kusini, tayari kuanza kutekeleza miradi ya maendeleo itakayowakwamua wananchi kutoka katika lindi la umaskini wa hali na kipato na kuanza kuwa na matumaini ya Sudan ya Kusini mpya, inayojikita katika maendeleo endelevu!

Vita, ghasia na mipasuko ya kijamii, chanzo chake kikubwa ni umaskini wa watu! Penye vita na baa la njaa, hapo umaskini na magonjwa yatapiga hodi kwa nguvu! Kardinali Peter Turkson anasema ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kuona misingi ya haki, amani na upatanisho vinatawala Barani Afrika, hususan huko Sudan ya Kusini na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati, ambao bado anaendelea kuwabeba katika sakafu ya moyo wake, kwani ameshuhudia kwa macho yake  mwenyewe mateso na mahangaiko ya familia ya Mungu na kiu ya kutaka kuanza kuandika upya ukurasa wa upatanisho na msamaha, ili kweli haki na amani viweze kutawala na hatimaye, kuchochea mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati yao kuhusu Kanisa katika ulimwengu mamboleo, wanasema, furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.