2017-07-01 17:04:00

Kardinali Sandri: Yaliyojiri wakati wa hija ya kitume nchini Bulgaria


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiri wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, kuanzia tarehe 29 Juni 2017 hadi tarehe 2 Julai 2017 amekuwa na ziara ya kikazi nchini Bulgaria kwa mwaliko wa Baraza la Maaskofu katoliki Bulgaria. Baada ya kuwasili nchini humo, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani walioyamimina maisha yao kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa nia ya kumwombea Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake.

Baadaye, alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Bwana Krasimir Karakachonav, Makamu wa kwanza wa Waziri mkuu ambaye pia ni Waziri wa ulinzi na usalama nchini Bulgaria. Mazungumzo yao, yamejikita kwa namna ya pekee kuhusu mchango unaoweza kutolewa na dini mbali mbali duniani katika kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na mataifa katika ujumla wake. Ni matumaini ya Kardinali Sandri kwamba, serikali ya Bulgaria, italitambua Kanisa kisheria na hivyo kuweza kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Bulgaria.

Kardinali Sandri pia amekutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa la Kirthodox la Bulgaria, chini ya uongozi wa Patriaki Neofit. Viongozi hawa wawili wamezungumzia kuhusu mchakato wa majadiliano ya kiekuemene baina ya Makanisa haya mawili. Wamekumbushia hija ya kiekumene iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Bulgaria pamoja na mikutano kadhaa waliyofanya na Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, wanaonesha moyo wa kuendeleza majadiliano ya kiekumene katika huduma, sala, maisha ya kiroho sanjari na ushuhuda wa uekumene wa damu, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Changamoto kwa wakati huu ni mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene ili kuwa na umoja kamili miongoni mwa wafuasi wa Kristo.

Kardinali Sandri pia amekutana na kuzungumza na Shekhe Mustafa Hazdi, Muft mkuu wa Bulgaria, ambao wamegusia kwa namna ya pekee kabisa mchango wa dini katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni wajibu wa dini kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana. Ni wajibu wa dini kudumisha amani duniani kwa kuwasaidia vijana kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na upatanisho. Kardinali Sandri amekutana, amesali na kuzungumza na wakleri na watawa mbali mbali nchini Bulgaria pamoja na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, tukio ambalo limehudhuriwa na viongozi wa Makanisa na Serikali ya Bulgaria pamoja na wanadiplomasia na wawakilishi mbali mbali wa serikali na mashirika yao ya kmataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican
All the contents on this site are copyrighted ©.