2017-07-01 16:03:00

Dumisheni tunu msingi za maisha ya ndoa na familia!


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuanzia tarehe 29 Juni hadi tarehe 2 Julai 2017 linaadhimisha Kongamano la shughuli za kichungaji linalojikita katika mradi mkubwa wa Fumbo la uzuri na utakatifu wa maisha ya Ndoa na Familia. Kongamano hili kwa namna ya pekee linajikita katika amana ya mafundisho ya Padre Renzo Bonetti. Linahudhuriwa na vyama mbali mbali vya maisha na utume wa familia. Lengo ni kuziwezesha familia ya Kikristo katika mazingira ya kifamilia kutambua na kuthamini zawadi ya maisha na utume wa ndoa na familia.

Kongamano la mwaka huu, 2017 linaongozwa na kauli mbiu “Kwa njia ya Neema ya Sakramenti ya Ndoa: Hata nyumbani ni rasilimali ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya uinjilishaji na ujenzi wa jumuiya”. Jumamosi asubuhi, tarehe 1 Julai 2017 Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa wajumbe waliokuwa wanahudhuria kongamano hili kwa kukazia umuhimu wa familia kuwa ni shule ya maisha inayoongozwa na Mwenyezi Mungu kwa kumwachia nafasi aweze kutenda kadiri ya mapenzi yake pasi na kumwekea vizuizi, ubinafsi na uchoyo mambo ambayo wakati mwingine, mwanadamu anapenda kuyang’ang’ania kwa nguvu sana hata kama hayana mvuto wala tija.

Monsinyo Viganò anakaza kusema, Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anafikiri na kutenda; anavyotekeleza ahadi zake kwa kuonesha ukuu na uweza hata kwa mambo ambayo kwa mwanadamu tayari alikuwa amekwisha yakatia tamaa kama ilivyokuwa kwa Abramu na mkewe Sara aliyekuwa mgumba na umri wake ulikuwa ni mkubwa. Abramu aliwezeshwa kuwa ni mwono mpana sana katika maisha yake, akafanikiwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, aliyemweka kuwa ni kiini cha maisha yake ya kila siku. Ukarimu kwa wageni unamwezesha Abramu kupata baraka na neema mbele ya Mwenyezi Mungu. Kilikuwa ni kitendo cha utovu wa nidhamu “kudadisi maisha ya mke wa jirani yako”. Lakini, Mwenyezi Mungu ni asili ya wema na maisha, ustawi na maendeleo ya mwanadamu ndiyo maana anajihusisha na masuala ya kifamilia na kwamba, hili ni jambo la wanafamilia wote, kwani Mwenyezi Mungu alikuwa anataka kuwajalia zawadi ya maisha, ili kutekeleza ahadi ya kumpatia Abramu uzao. Hii ni changamoto kwa familia kutoa nafasi itakayoweza kumkirimia Mungu ili aweze kuishi na kukaa kati yao!

Hii ni changamoto kubwa kwa watu wa nyakati hizi kwamba, wanapenda kumzuia Mwenyezi Mungu kwa kupandikiza mbegu ya kifo, dhidi ya utamaduni wa maisha. Waamini waoneshe ukarimu katika imani kwa kujiweka na kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu kama alivyofanya Abramu na mkewe Sara. Matokeo yake, Sara akawa ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa yale mambo ambayo walidhani kwamba, hayawezekani kabisa kwa macho ya kibinadamu, lakini mbele ya Mungu yamekuwa ni chemchemi ya furaha, kielelezo cha ukuu na uweza wa Mungu. Pale mwanadamu anapoungama udhaifu na dhambi zake, Mwenyezi Mungu anamsaidia na kumwinua kutoka mavumbini. Kumbe, mambo msingi ya kuzungatia katika maisha na utume wa ndoa na familia ni kukuza na kudumisha upendo na ukarimu; imani na matumaini; umoja na mshikamano katika kuamua, kupanga na kutekeleza majukumu mbali mbali ya maisha na utume wa familia kama alivyofanya Abramu na Sara mkewe!

Monsinyo Viganò anakaza kusema, kuna haja ya kuwa na uelewa na mwelekeo mpana zaidi kuhusu maana halisi ya familia inayojikita katika udugu, upendo, ukarimu na huduma kwa wageni, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuandaa mazingira yatakayosaidia familia kuwa kweli ni nyumba ya upendo; mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vinaheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Familia ni mahali ambamo tunu hizi msingi zinamwilishwa na kushuhudiwa kama sehemu ya mchakato wa kutangaza Injili ya familia kwa watu wa Mataifa.

Familia ni mahali pa malezi na majiundo ya awali, endelevu na makini; mahali ambapo wanafamilia wanaweza kusaidiana kwa hali na mali; wakasahihishana na kusameheana na kuchukuliana jinsi walivyo kwa yale yanayowaunganisha bila kusahau yale ambayo pengine yanawatofautisha. Familia ni mahali pa ujenzi wa upendo na mshikamano unaowaambata wote, kwani mwanadamu kabla hajafa hajaumbika, kumbe hatika safari ya maisha anaweza kukumbana na changamoto pamoja na mambo mbali mbali ya maisha.

Familia ni mahali pa kutangaza na kushuhudia huruma, msamaha na upatanisho; mahali ambapo mwanafamilia anaweza kuanza upya pasi na kutengwa wala kudhalilishwa utu na heshima yake, wala kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na athari za utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, familia ni chemchemi ya Habari Njema ya Wokovu na kamwe si mzigo na wala tatizo. Familia ni fursa inayopaswa kukuzwa na kudumishwa; kulindwa na kuendelezwa;  kwani ni baraka na chemchemi ya neema kwa binadamu; “oasisi ya upendo na matumaini”. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, kweli Injili ya familia inakuwa ni dira na mwongozo wa ya Kikristo. Ndani ya familia watu wanajifunza: ukweli na uwazi; huruma na upendo; faraja wakati wa mateso, mahangaiko na magumu ya maisha. Hakuna mwandani wa familia unaoweza kutoa mwongozo sahihi wa maisha, bali maisha ya kifamilia ni uzoefu na mang’amuzi yanayojengeka kila siku ya maisha. Hii ni dhamana isiyokuwa na mbadala hata kidogo.

Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza wanandoa na familia kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Hapa familia zinajiunda kuwa kweli ni shule ya utu na heshima ya binadamu; chachu ya huruma, upendo, mshikamano na ukarimu; shule inayowakumbatia na kuwaambata walimwengu wote pasi na ubaguzi. Hawa ni maskini, watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wote hawa wanapaswa kulindwa, kutunzwa na kudumishwa na familia. Ikumbukwe kwamba, familia ni mlango wa neema, baraka na huruma ya Mungu kwa waja wake. Familia ziwe kweli ni mlango wa imani, matumaini na faraja na kamwe watu wasichoke kuziendelea familia za Kikristo ili kupata faraja, huruma na kuonja upendo.

Monsinyo Viganò anakaza kusema: familia ni shule ya maisha, elimu ya udugu, ukarimu na upendo; ni mahali pa huruma na faraja; mahali pa kujitoa kimasomaso bila ya kujibakiza, mwaliko kwa wanandoa na familia kutafakari kwa kina na mapana Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilivyo ng’ara kwa imani, upendo na matumaini, ili kweli familia ya binadamu iweze kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani; mahali pa sala, na upendo; kamwe familia zisiwe ni vichaka vya ghasia, vipigo na nyanyaso kutokana na aina mbali mbali ya mifumo ya kifamilia. Familia iwe ni kimbilio la wakosefu, wale wanaotaka kugangwa na kuponywa; iwe ni chemchemi ya utakatifu wa maisha kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
All the contents on this site are copyrighted ©.