2017-07-01 17:20:00

Dumisheni moyo wa upendo na ukarimu!


Ndugu msikilizaji karibu katika kipindi chetu cha tafakari ya Neno la Mungu, kutoka matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. Tupo katika Dominika ya 13, Mwaka A wa Kanisa, na kadiri ya masomo ya leo, nakualika tuielekeze tafakari yetu katika fadhila ya ukarimu na thawabu zake katika maisha yetu ya kiroho kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, Ufalme unaosimikwa katika haki, amani, upendo na mshikamano. Basi naomba nikualike ujikusanye na kumkaribisha Roho Mtakatifu atuongoze katika tafakari yetu.

Ndugu msikilizaji, ukarimu ni ile hali ya kujitoa, kujisadaka kwa ajili ya wengine. Kila mmoja ana mahitaji ambayo kwa namna moja au nyingine atawategemea wengine ili kukidhi mahitaji yake. Wakati huo huo kila mmoja ana kitu ambacho anaweza kumuwezesha mwingine katika mahitaji yake. Yamekuwa ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwamba binadamu wasaidiane kwa ukarimu katika maisha ya kila siku. Hivyo haidhuru hitaji la mtu ni dogo au kubwa kiasi gani, na haidhuru alicho nacho mtu ni kingi au kidogo kiasi gani. Cha msingi ni moyo wa ukarimu.

Nabii Elisha tunamsikia akiwa Shunemu, anapata hifadhi na huduma ya chakula kutoka kwa mwanamke mmoja ambaye alikuwa ni mtumishi mwenye cheo katika jamii. Mwanamke huyo alikuwa mkarimu kwa Elisha kabla hajafahamu kuwa Elisha alikuwa nabii. Baada ya ushuhuda wa mwenendo wa maisha ya Elisha, ndipo anagundua kuwa ni zaidi ya mtu tu mwenye shida, mtu mhitaji wa hifadhi, ndipo anamwambia mumewe: Sina shaka kwamba mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu (Rej., 2Wafalme 4:9). Hudumia kwa ukarimu watu wahitaji bila ubaguzi wa huyu ni nani au anayo nafasi gani katika jamii, au ana mahusiaono gani nawe, au unamfahamu au humfahamu.

Katika historia ya mwanadamu, kwa muda mrefu sana, ilikuwa ni jambo la kawaida kila ukutanapo na mtu anayeonekana myonge au anayeomba msaada, alikuwa kweli mhitaji kwa nia njema. Ingawa hata karne zilizopita kumekuwa na changamoto za uaminifu na wema, kwa miaka ya hivi karibuni, suala la ukarimu na uaminifu limekuwa gumu zaidi, kwani kumekuwa na utapeli mwingi, kumekuwa na dhuluma sana, udanganyifu umeijaa mioyo ya wanadamu wengi. Watu wengi wanataka kutumia ukarimu na wema wa wengine kuwanyonya, kuwatapeli, kufaidika au hata kuwatendea mabaya.

Sasa tabia kama hizi, zimepelekea wengi kusita kuwa wakarimu au kutenda wema. Bila shaka nawe ndugu msikilizaji, mahali fulani umesita kutenda ukarimu au wema kwa kuhofia kutendewa vibaya, au kunyonywa sababu watu wanataka kutumia wema wako kujinufaisha. Kuna nyakati zingine umeshindwa kutenda ukarimu kwa kuogopa kusemwa au kudhaniwa vibaya. Hii ni sababu binadamu wengi leo, wanatenda ukarimu au kuonesha wema sababu wanajua watapata faida fulani. Lakini swali linabaki: Je! tutasita mpaka lini kutenda ukarimu; Je! wale wahitaji kweli waachwe katika shida na mahangaiko yao sababu ya woga na hofu uliyo nayo; Je! wewe usipotenda ukarimu utapataje thawabu. Kumbuka kwamba kutenda ukarimu kuna thawabu zinazoambatana nazo.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican,  ngoja nikutobolee siri sasa ya jambo hilo ili upate majibu sahihi ya maswali hayo. Ni kweli kwamba huwezi kujiachia kwenye ukarimu na wema ukawaacha watu wakafaidika na kuutumia vibaya wema wako, hata kukuumiza. Tabia za janja ya nyani kula hindi bichi zimekuwapo tu karne zote. Kristo analitambua hilo ndio sababu anakutahadharisha: nawatuma ninyi kama kondoo kati ya mbwa mwitu. Muwe welevu kama nyoka, na wapole kama njiwa (Rej., Mathayo 10:16). Ndugu katika Bwana, sijui umewahi kutafakari kiasi gani lugha hii ya picha anayoitumia Mwalimu wa walimu, Mjanja wa wajanja.

Nyoka ni kiumbe anayekwenda kwa kutambaa chini na pengine unawezakudhani ni rahisi sana kumkanyaga, lakini utagundua hilo huwa gumu sana, kwani nyoka ni mwepesi sana kuhisi hatari inapomsogelea, na akiishahisi hatari hiyo hunyanyua kichwa kujihami. Kama ipo hatari huwa anakwepa, ingawa hulazimika kuigonga hatari hiyo wakati mwingine. Sasa Kristo anakualika kuwa mwelevu kwenye kuhisi hatari mapema, na kuwa makini kutoathirika na wale wenye nia mbaya na ukarimu wako. Hata hivyo, badala ya kujibu mashambulizi kama nyoka, anakualika uwe mpole kama njiwa. Njiwa kwa tabia atatishwa, atafukuzwa, atapondwa lakini huwa mpole na kuendelea kuzungukazunguka maeneo hayo bila kutema sumu, bila tusi, bila kushambulia mtu au hatari inayomkabiri. Uwe mpole kuendelea kutenda ukarimu na wema bila kurudi nyuma, wala kulipa kisasi kwa waliowahi kukuingiza kwenye hatari, lakini kuwa tu makini, wagundue mapema, na kwepa mbinu zao wasijekukutenda.

Ukidumu katika kutenda ukarimu, Mungu naye atakujibu katika mahitaji yako kwa thawabu kadiri ya unavyotenda ukarimu. Ushasikia bila shaka kale ka msemo kwamba: mwenye kutoa kwa ukarimu huongezewa. Unaweza ukawa wewe pia una shida fulani, lakini mwingine ana shida kubwa zaidi, katika mazingira kama hayo, usiwe mchoyo, usiipende zaidi nafsi yako kuliko shida kubwa za wengine, usiwapende sana ndugu zako na kuwajali kuliko wengine wenye shida zaidi. Kristo asema: apendaye baba au mama kuliko mimi hanistahili, wala apendaye mwana au binti kuliko mimi hanistahili (Rej., Mathayo 10: 37). Kristo hamaanishi usiwajali watu wako wa karibu, la hasha, anachomaanisha usiwe na tabia ya ubaguzi, ukaacha mtu mwenye shida kubwa ukamjali ndugu au nafsi yako kwa jambo ambalo sio la lazima. Jali na kirimia watu kadiri ya shida na mahitaji yao, sio sababu ya undugu au kufahamiana.

Ndugu msikilizaji, unapotoa kwa ukarimu, Mwenyezi Mungu pia atakukirimia thawabu kadiri ya ukarimu huo. Unapokuwa na mkono wa birika, ulichonacho hakitakutosha na wala hutapata thawabu yeyote. Unapokuwa mkarimu katika mambo ya afya, kwa wakati muafaka atakukirimia thawabu ya afya au matibabu, ukiwa mkarimu katika haki, kwa wakati muafaka utapata thawabu inayoendana na sheria na haki, ukiwa mkarimu kutafuta upatanisho na amani, kwa wakati muafaka utapata thawabu ya amani, ukiwa mkarimu katika uaminifu, Mwenyezi Mungu atakukirimia thawabu ya uaminifu. Kuwa mkarimu na utaona ahadi ya Kristo kwako ilivyo ya kweli, kwa hakika haitakupotea kamwe thawabu yako.

Tunapoelekea kuahirisha tafakari hii kwa leo, nikutahadharishe tu jambo moja la msingi sana kwamba, katika ukarimu wako, uwe mkarimu kwa nia njema, na kwa kuzingatia maadili na haki. Usiwe mkarimu kwa matarajio ya kupata kitu kutoka kwa unayemtendea ukarimu, au kwa kutumia mali ya watu wengine kuwadhulumu au kuwaonea, wala usiwe mkarimu kupitia njia ambazo ni dhambi. Ukarimu unapaswa uwe wa haki na uadilifu. Shukrani za dhati ziwaendee Sr. Maxmilliana Massawe na Padre Richard Mjigwa kwa ushirikiano wao mzuri katika maandalizi ya kipindi hiki. Nakushukuru pia ndugu msikilizaji kwa kuwa nami katika tafakari hii. Tuonane tena panapo majaaliwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa jina ni Padre Celestine Nyanda, na kwa sauti ya kinabii nakuaga nikisema TYK, LIC! 
All the contents on this site are copyrighted ©.