2017-06-30 16:17:00

Papa Francisko: Dumisheni maendeleo, ratibuni rasilimali & jadilini!


Shirikisho la Italia na Amerika ya Kusini lililoanzishwa miaka 50 iliyopita lilikuwa linapania kukuza maendeleo endelevu na kuratibu shughuli za ukuaji wa uchumi ambazo zingeweza kutekelezwa kwa pamoja na nchi wanachama. Baada ya miaka 50 ya uwepo na huduma zake, kuna haja ya kukazia mambo makuu matatu: kwanza kabisa ni kutambua umuhimu wa kudumisha maendeleo endelevu, pili ni kuratibu rasilimali zilizopo ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo na tatu ni kuendeleza utamaduni wa majadiliano ya kisiasa na kiuchumi ili kudumisha amani duniani.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 30 Juni 2017 alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Italia na Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu anasema, nchi za Amerika ya Kusini zimebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa historia, tamaduni na rasilimali asilia pamoja na rasilimali watu ambao kweli ni wema na wanapenda kushirikiana na watu wengine. Mwelekeo huu umejionesha kwa namna ya pekee wakati nchi za Amerika ya Kusini zilipokumbwa na majanga asilia.

Mshikamano huu umekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na Jumuiya ya Kimataifa. Lakini, mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa umeendelea kusababisha ongezeko kubwa la umaskini, ukosefu wa fursa za ajira; mpasuko wa kijamii ambao umekuza pengo kubwa kati ya maskini na matajiri. Changamoto hizi zinahitaji upembuzi yakinifu utakaotoa kipaumbele cha kwanza kwa watu halisi! Kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kutambua matatizo, changamoto na fursa zilizopo sanjari na kuthamini utajiri unaofumbatwa katika maisha ya kila mtu na jamii ya watu katika ujumla wake!

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuratibu rasilimali zilizopo ili kuweza kukidhi mahitaji msingi ya wananchi wa Amerika ya Kusini. Kuratibu ni mchakato unaohitaji rasilimali muda na nguvu kwani hii ni kazi iliyofichama na wakati mwingine inaangaliwa kwa “jicho la kengeza”, lakini ni muhimu sana. Katika ulimwengu wa utandawazi na kama ilivyo hali changamani huko Amerika ya Kusini, kuna haja ya kuunganisha nguvu ili kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, kwa kutibu chanzo chake hata kama muda umepita sana, lakini bado hawajachelewa hata kidogo. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ambalo halijawahi kutokea duniani katika miaka ya hivi karibuni.

Wananchi wa Amerika ya Kusini wanasukumizwa na changamoto za maisha kutafuta “oasis” za matumaini, ili kuweza kupata uhakika na usalama wa maisha yao; fursa za ajira ambazo zitawasaidia kukuza na kudumisha utu na heshima yao kama binadamu! Katika hali na mazingira kama haya, watu wengine wanajikuta wakiwa wanapoteza haki zao msingi; watoto na wanawake wanatumbukizwa katika biashara ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo; wananyanyaswa na kudhulumiwa! Kuna wakati wanajikuta wametumbukia katika mtandao wa magenge ya kihalifu. Matokeo yake ni kusambaratika kwa familia; wengi wao wanajikuta wakiwa mbali na nchi zao asili na kwamba, hata serikali zenyewe mara nyingi zinajikuta zikiwa zimegawanyika kufuatia wimbi la wakimbizi na wahamiaji duniani!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuliwa katika medani za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Wananchi wamechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo yao, lakini kwa bahati mbaya wanaendelea kunusa harufu mbaya ya saratani ya rushwa na ufisadi kutokana na ugawaji pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali za nchi husika. Wananchi wanataka kusimama kidete kujenga jamii inayosimikwa katika haki ili kudumisha utawala wa haki na sheria. Kumbe, ukuzaji wa majadiliano ya kisiasa ni jambo muhimu sana katika uwanja wa Jumuiya ya Kimataifa, lakini kwa namna ya pekee na Bara la Ulaya kutokana na mahusiano ya tangu awali.

Baba Mtakatifu anasema, majadiliano haya hayana budi kusimikwa katika diplomasia kama chombo msingi na mshikamano kama njia ya kufikia mchakato wa amani. Majadiliano ni muhimu, lakini si sana katika majadiliano ya masuala ya fedha, kwani hapa kuna haja ya kuwa makini kuweza kupokea ushauri unaotolewa na wengine ili kushirikishana matunda yake. Majadiliano hayana budi kusimikwa katika uaminifu kwa kutambua na kuheshimu utu wa jirani anayeomba msaada na kutamani kuona akitendewa wema ili kukuzana kudumisha mafungamano ya kidugu na kirafiki ili kudumisha misingi ya haki na amani. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia wajumbe hawa utekelezaji wa dhamana yao kikamilifu kwa ajili ya ustawi wa wengi, huko Amerika ya Kusini. Ushirikiano na mshikamano usaidie mchakato wa ujenzi wadunia inayosimikwa katika udugu na haki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.