2017-06-30 09:57:00

Onesheni ukarimu ili kujenga Ufalme wa Mungu!


Ndugu mpendwa, karibu tutafakari pamoja neno la Mungu dominika nyingine ya mwaka, dominika ya 13.  Dominika iliyopita tulitafakarishwa na kusikia habari juu ya ufalme wa Mungu na kualikwa kushiriki kikamilifu katika kueneza ufalme wa Mungu, tena bila woga. Mwaliko utokao katika Neno la Mungu dominika hii ya leo ni wito wa kuwa na roho ya ukarimu na katika kuishi wito huu, tunaambiwa kuwa itakuwa rahisi kuishi upendo mkuu wa Mungu kwetu. RealAudioWito wa Mungu kwetu ni kumtumikiaYeye na watu wake. Ni katika kumpenda na kumtumikia Mungu, mkristo anaweza kutoa huduma kwa wengine na kwa njia hiyo kuendelea kumpokea Mungu zaidi na zaidi. Basi katika kutenda hayo, Mungu anatangaza uhakika wa thawabu kwa mwenye kutenda hilo. Yule anayetenda katika upendo na katika roho ya ukarimu atapata Baraka.

Mpendwa, katika somo la kwanza toka kitabu cha Pili cha Wafalme tunakutana na Nabii Elisha akiwa katika nchi ya Shunemu. Huu mji ulijengwa kando ya mlima na wakazi wake walijiweza kiuchumi. Nabii Elisha alikuwa akipita eneo hilo mara kwa mara. Katika mojawapo ya familia za mji huo alikuwepo mwanamke tajiri lakini tasa.  Katika ukarimu wao wanamkaribisha Elisha nyumbani kwao na ndipo baadaye wanagundua kuwa ni nabii wa Mungu. Wanampatia malazi katika nyumba yao na katika ukarimu wao huo wanajaliwa mtoto. Wanapata zawadi takatifu ya Mungu. Katika mazingira ya wakati huo, mtu wa Mungu alimwakilisha Mungu Mwenyewe na hivyo alistahili heshima kubwa.

Katika somo la Pili Mtakatifu Paulo anawaandikia Warumi akiwakumbusha maana ya ubatizo, kwamba sisi ni watu wa ubatizo  na kwamba baada ya ufufuko kama Bwana alivyo mtakatifu, nasi tunaalikwa kuenenda katika upya wa maisha, yaani ule upya tulioupata kwa njia ya Neema ya Utakaso. Ni katika mantiki hiyo ya ufufuko nasi tutaishi milele pamoja na Kristo. Jibu la mwanadamu kwa tendo hili takatifu ni kutambua huo upendo wa Mungu na kushiriki kiaminifu katika kumtumikia huyo Mungu aliyetuumba na kutukomboa sisi.

Katika Injili ya Mathayo, Bwana anafundisha namna mbatizwa ambaye amekufa katika mauti na Bwana na kufufuka naye anavyopaswa kuishi upendo. Upendo wake unapaswa kuwa  upendo uliojaa huduma kwa wengine. Tumeona katika somo la kwanza – nabii Elisha akitoa ushuhuda na akihudumia na akihudumiwa na katika somo la pili Mtume Paulo akitukumbusha kuhusu ubatizo wetu na hadhi tuliyonayo. Sisi tuliobatizwa katika jina la Bwana, tunaalikwa kushuhudia upendo huo kwa ukarimu, tukiwasaidia wengine waweze kumjua Bwana na watu wake. Na hapa tunaona wazi wito wa kumpenda Mungu kwa upande mmoja na kwa upande mwingine haja ya kutoa huduma kwa watenda kazi wake. Dhamira hii ya ukarimu inakaziwa katika liturjia ya leo kwani ndiyo inayotuongoza. Hata katika injili tunaona msemo wa Yesu – anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma…

Ndugu yangu, upendo wa kweli wa mtu kwa Mungu unapaswa kuwa upendo uliojaa huduma kwa wengine. Upendo ambao Bwana anautaka ni ule ambao unahudumia walio wahitaji na walio katika huduma ya Neno la Mungu. Sehemu ya kwanza ya Injili inasema wazi, anayetaka kunifuata na kuuishi upendo hana budi kuwa huru na vifungo vyo vyote vile.

Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu ni hitimisho la hotuba ya kimisionari kama ilivyo katika Mat. 9:35-11:1 kama ilivyoanza na utume wa mitume. Katika hotuba hii, Yesu anawaambia mitume jinsi watakavyoenenda na habari kuhusu matumaini yao. Aidha, wanakumbusha kuwa migawanyiko inayoonekana katika familia, inaweza kuwakumba pia mitume katika utume wao. Katika sehemu  ya pili  ya Injili hii, Bwana anakazia suala la shukrani kwa watoa huduma, yaani watenda kazi katika shamba lake. Anasema, atendaye mema kwa hawa watumishi anitumikia mimi. Mkristo anakumbushwa haja ya kushiriki kueneza utume na upendo huo kwa hali na mali. Tunakumbushwa kuwa wajibu wa kueneza ufalme wa Mungu ni wetu sote nasi hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kutupatia nafasi ya kushiriki katika kueneza upendo huo. Ni wajibu wetu sote kushiri kiaminifu katika kueneza upendo huu kwa ukarimu wetu wote. Ieleweke wazi kuwa hoja kuu ni kushiriki kwa ukarimu katika utume wa Mkombozi wa ulimwengu yaani Bwana wa mavuno mwenyewe.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.