2017-06-29 14:09:00

Mwamini kiri imani na kumbatia mateso kwa nguvu ya sala


Liturujia ya maadhimisho ya sikukuu ya Watakatifu Petro na Paulo inatoa maneno matatu ya msingi sana kwa maisha ya mtume. Maneno hayo ni kukiri, mateso na sala. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyoanza mahubiri yake, wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu kwa heshima ya sikukuu ya Watakatifu Petro na Paulo, maadhimisho yaliyofanyika tarehe 29 Juni 2017, katika uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.

Petro anakiri imani, pale ambapo Bwana Yesu analigeuza swali kutoka kwenye ujumla na kulifanya kuwa binafsi. Swali la Bwana lilikuwa ni juu ya kile ambacho watu husema kuwa Yeye ni nani. Kwa mtazamo wa haraka wa majibu, alifahamika kama nabii kati ya watu. Swali lilipokuwa binafsi kwa mitume wake kuwa wao wanamfahamu kama nani, Petro anakiri kumtambua kuwa ni Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kukiri imani maana yake ni kumtambua Yesu kuwa ndiye Masiha aliyesubiriwa kwa muda mrefu sana, Mungu aliye hai, Bwana wa maisha na uzima wa kila binadamu.

Swali hili leo linamwelekea kila mwamini, kila binadamu, na zaidi sana watumishi wa Mungu. Jibu la swali hili haliwezi kuwa la juu juu tu. Ni jibu linalohitaji kujitosa kimaisha, kwani ni swali linalogusa maisha ya mtu, kumtambua na kumkiri Muumba wako, Bwana wa uzima wako, Bwana wa maisha yako, sababu ya matumaini yako, hamu ya moyo wako, chemchemi ya uaminifu wako. Waamini lazima wahame na swali hilo kutoka kwenye ujumla wake na kuwa swali binafsi, kasha watoe jibu binafsi, sio tu kwa maneno bali kwa matendo katika maisha ya kila siku.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujiuliza kama ni wafuasi wa Kristo kisaniisanii kwa kuchat na kumung’unya tu ubuyu kuhusu yale yanayoendelea duniani, au ni wafuasi walio katika hija ya kushuhudia kweli imani iliyo thabiti, na wanaoishi na Kristo mioyoni mwao. Anayemkiri Kristo hatoi maoni tu na kuishia kupapasapapasa mwenendo wa maisha kana kwamba kunywa maji, bali ni mtu anayetoa maisha yake kwa kutweka mpaka kilindini kama walivyofanya mitume Petro na Paulo, waliyamimina maisha yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo na kwa ajili ya ndugu zao. Kumbe ufuasi wa Kristo, ni ufuasi unaopitia njia ya mateso, msalaba na ndipo hupatikana furaha ya ufufuko.

Waamini wa Kanisa la awali pia waliteswa sana kama inavyosimuliwa katika kitabu cha matendo ya Mitume. Leo hii waamini katika jumuiya mbali mbali duniani wanateswa, wananyanyaswa, wanabaguliwa, wanatengwa na kuuwawa, hali wale wenye uwezo na wajibu wa kuingilia kati na kutetea haki zao, wamekaa kimya wakishuhudia hali inavyozidi kuwa mbaya. Mtakatifu Agustino anafundisha kwamba fadhila ya ukristo sio tu kutenda wema, bali pia kuvumilia mabaya, kama alivyofanya Kristo na ndio mwaliko kwa waamini wote, wakitambua kuwa Kristo yupo pamoja nao siku zote. Kwa namna hii watakuwa na ujasiri wakusema pamoja na Mtume Paulo: daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi, twapata mashaka lakini hatukati tamaa, twateseka lakini hatuachwi bila msaada, na ingawa tumeangushwa chini, hatukuangamizwa (Rej., IIWakorintho 4: 8-9).

Kuvumilia nyanyaso na aina zote za uonevu ni kushinda uovu pamoja na Kristo, na kwa namna ya Kristo Mwenyewe, ambayo sio namna ya dunia hii. Huu ni ushindi unaohitaji kuilinda imani thabiti, hata kama afya inayumbishwa na hata kama kunakusongwa na ubaya wa wengine ili kumkatisha mwamini tamaa. Mwamini anaishi kwa ajili ya Kristo, na kwa ajili ya ndugu zake, na sio kwa ajili yake mwenyewe. Hivyo anakaza mwendo kila siku kulielekea lile taji atakalokabidhiwa kwa wakati muafaka, ili aweze kuimba utenzi wa ushindi pamoja na Mtume Paulo: nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda (Rej., IITimotheo 4:7).

Katika hali kama hizo, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza waamini na kwa namna ya pekee kabisa wachungaji wenye Daraja Takatifu, kujikita katika maisha ya sala, kwani sala ni kama maji yanayohitajika kunyunyizia matumaini na kukuza imani. Imani inamfanya mfuasi wa Kristo kujisikia kupendwa na hivyo kujifunza kupenda wengine. Katika sala mwamini anaweza kuwa mvumilivu katika mateso na mahangaiko mbali mbali ya maisha. Sala zifanyike pia kuwaombea wengine hasa wale wanaoteseka zaidi. Hata Petro alipokuwa gerezani Kanisa lilikuwa likimuombea kwa moyo (Rej., Matendo 12:5). Bila sala, vifungo vya ndani vya mwamini haviwezi kufunguka. Waamini wakiwa watu wa sala watakuwa na maisha yenye amani siku zote.

Kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu Francisko, kawatia moyo maaskofu wakuu wapya 36, ambao wamepewa Pallio Takatifu ili wawe kweli wachungaji wema wa kubeba kondoo mabegani mwao, kwa mfano wa Kristo mwenyewe katika majimbo makuu waliyokabidhiwa kuwa ishara ya umoja na udugu. Kati yao maaskofu wakuu 8 ni kutoka Afrika:

Askofu mkuu Antony Muheria kutoka Jimbo kuu la Nyeri, Kenya.

Askofu mkuu Inàcio Saure, kutoka Jimbo kuu la Nampula, Msumbiji.

Askofu mkuu Paul Desfarges, kutoka Jimbo kuu la Algeria, Algeria.

Askofu mkuu Michael Didi Adgum Mangoria, Jimbo kuu la Khartoum, Sudan K.

Askofu mkuu Fridolin Ambongo Besungu, Jimbo kuu la Mbandaka, DRC.

Askofu mkuu Faustin Ambassa Ndjodo, Jimbo kuu la Garoua, Cameroon.

Askofu mkuu Goetbe Edmond Djitangar, Jimbo kuu la N’Djamena, Chad.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.