2017-06-29 10:03:00

Makardinali wapya wamtembelea Papa Mstaafu Benedikto XVI


Makardinali wapya wanapaswa kuyaelekeza macho na mawazo yao kwenye Fumbo la Msalaba, wa mahangaiko ya watu wa Mungu kwa nyakati hizi. Hawa ndio wale wanaoteseka kwa vita, ghasia, vitendo vya kigaidi, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo inayonyanyasa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni wajibu wao kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu! Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 28 Juni 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro katika Ibada ya kuwasimika Makardinali wapya watano, ambao sasa ni sehemu ya Baraza la Makardinali ambalo lina dhamana ya kumshauri Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Juan José Omella, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcelona, nchini Hispania kwa niaba ya Makardinali wenzake, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwateuwa kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa la Kristo kama washauri wakuu, kiasi hata cha kuweza kujisadaka kama itabidi kwa ajili ya imani na maadili ya Kanisa kama ambavyo aliwahi kusema, Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Hii ni dhamana nzito inayodai ushuhuda wa imani kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kristo, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo hasa miongoni mwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Vazi jekundu wanalovaa Makardinali ni alama ya ushuhuda wa hali ya juu kabisa kwamba, wamekombolewa kwa njia ya Damu Azizi ya Kristo Yesu; alama na wito wao unaowadai kutupilia mbali matamanio ya kibinadamu, ili kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu na uamianifu kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro hapa duniani. Hawa ni Makardinali kutoka katika nchi tano tofauti zinazofumbatwa katika ushuhuda na uaminifu kwa Injili. Baadhi ya Makardinali wanatoka katika mazingira magumu ya vita na umaskini na sasa wanaitwa kuwa watetezi wa Injili ya maskini na kwamba, matumaini ya watu wa Mungu yanafumbatwa katika nyoyo zao.

Makardinali kutoka katika sakafu ya mioyo yao wanataka kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani wakisema: Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo. Kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. (Rej. Ef. 1: 3-4). Makardinali wanakiri kwamba, wito na utume huu ni neema na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ndiyo maana wanataka hata wao kujisadaka na kujimega kama Ekaristi Takatifu kwa Baba wa milele katika huruma ya Kristo na Roho Mtakatifu.

Makardinali wanakaza kusema, hii ni huduma inayotekelezwa katika furaha na matumaini kwa Kristo Yesu na wanatambua kwamba, zawadi hii inahifadhiwa katika chombo cha udongo na zaidi ya hayo, wanawajibishwa na upendo wa Kristo. Wanataka kuwa sehemu ya Kanisa linalosafiri linalojitaabisha kuwatafuta watu wote, kwa kuwaganga na kuwatibu kwa mafuta ya furaha na amani; kwa kupangusa machozi ya watu kwa Injili ya matumaini na upatanisho unaobubujika kutoka kwa Mwana mpendwa wa Mungu. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awasogeze Makardinali wapya karibu zaidi na Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kuwaonesha Uso wa Yesu kwa binadamu wanaohitaji faraja!

Makardinali wakiwa wameambatana na Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Ibada ya kuwasimika, walikwenda moja kwa moja kwenye Monasteri ya “Mater Ecclesiae” kumsalimia na kumtakia heri na baraka Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.