2017-06-27 15:44:00

Makardinali wapya kusimikwa, Jumatano tarehe 28 Juni 2017


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 28 Juni 2017, kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Ulaya ataadhimisha Mkutano wa Makardinali na kuwasimika Makardinali wapya watano kutoka katika Mabara matano. Hawa sasa wanajiunga na Baraza la Makardinali ambalo lina dhamana ya kutoa ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kwa Kanisa la Kiulimwengu. Makardinali wapya ni:

Kardinali Jean Zerbo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bamako, Mali.

Kardinali Juan Jose Omella, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcelona, Hispania.

Kardinali Anders Arborelius, Askofu wa Jimbo Katoliki la Stockholm, Sweden.

Kardinali Louis-Marie Ling Mangkhanekhoun, Askofu wa Laos, Cambodia.

Kardinali Gregorio Rosa Chàvez, Askofu msaidizi Jimbo kuu San Salvador, El Salvador.

Baba Mtakatifu tangu wakati alipowateua, aliwaweka Makardinali wateule chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani, ili wasaidie mchakato wa kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na kwamba, ushauri wao uweze kuwa na tija katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Makardinali wapya wataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 29 Juni 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu atabariki pia Pallio Takatifu, watakazovikwa Maaskofu wakuu walioteuliwa katika kipindi cha Mwaka 2016 – 2017 kwenye Majimbo yao Makuu. Dhamana hii itatekelezwa na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika.

Hadi sasa Bara la Ulaya linaongoza kwa kuwa na Makardinali 109, kati yao wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura ni 53. Amerika ya Kaskazini ina Makardinali 26, kati yao wenye dhamana ya kupiga na kupigiwa kura ni 17. Amerika ya Kati ina jumla ya Makardinali 9 kati yao Makardinali 5 wanaweza kupiga na kupigiwa kura. Amerika ya Kusini ina jumla ya Makardinali 26 kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura ni 12. Bara la Afrika lina jumla ya Makardinali 25 kati yao wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura ni 15. Bara la Asia lina jumla ya Makardinali 24, wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura ni 15, mwishoni ni Oceania ambayo ina Makardinali 6 kati yao wenye haki ya kupiga kura ni 4.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.