2017-06-26 15:06:00

Wakristo msibweteke! Chakarikeni ili kukutana na Mwenyezi Mungu!


Mkristo wa kweli anapaswa kuonesha machachari yake kwa kutoka ili kumtafuta na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kamwe asikubali kubweteka na kukaa kitako. Anapaswa kutenda kama alivyofanya Abramu, Baba wa imani aliyekubali kumtii Mwenyezi Mungu na kuanza safari kuelekea kwenye nchi ya ahadi. Mambo makuu matatu yanajionesha kwa Abrahamu yaani: kujivua kutoka katika nchi, tamaduni na mambo aliyoyapenda; pili ni kuanza kuelekea katika nchi ya ahadi iliyojaa maziwa na asali na tatu ni baraka inayofumbatwa katika maisha ya Abramu. Mwenyezi Mungu alimwamuru Abramu kutoka katika nchi yake, na jamaa zake na nyumba ya baba yake ili aende mpaka katika nchi atakayooneshwa na Mwenyezi Mungu.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 26 Juni 2017. Tabia ya kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza kama ilivyooneshwa na kushuhudiwa na Abramu inapata utimilifu wake kwa Kristo Yesu, aliyeyamimina maisha yake kwa njia ya mateso na kifo pale juu Msalabani, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwaliko wa kuacha nchi, jamaa na nyumba ni changamoto ambayo hata Manabii walipewa na Mwenyezi Mungu ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu. Ni watu ambao walikaza uso na kusonga mbele pasi na kurudi nyumba ili kuagana na ndugu na jamaa zao. Abramu alionesha utii mbele ya Mwenyezi Mungu, akawa kweli ni chemchemi ya matumaini ya ahadi za Mungu katika maisha yake. Hata leo hii, Mkristo hawezi kuongozwa n ana utabiri wa nyota, jambo la msingi ni kujisadaka na kujiaminisha mbele ya Mwenye Mungu, tayari kuanza safari ya kuelekea kwenye nchi ya ahadi ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwapatia kama urithi wao.

Mzee Abramu hakuwa na makazi ya kudumu, hali inaonesha kwamba, daima alikuwa ni msafiri mbele ya Mwenyezi Mungu na badala yake anamjengea Mungu Altare ili kumwabudu, kumtukuza, kumsifu na kumshukuru kwa wema na ukarimu wake usiokuwa na kifani! Hii ni hija ya matumaini inayofumbata ahadi za Mwenyezi Mungu katika maisha ya mwanadamu! Mshangao huu anasema Baba Mtakatifu Francisko, wakati mwingine, unamwacha mwamini akiwa amepigwa na bumbuwazi, kwani ni mshangao unaoweza kusababisha kifo, magonjwa; lakini pamoja na yote haya mwamini hana budi kuwa namatumaini kwamba, Mwenyezi Mungu atampeleka na kumfikisha kwenye bandari salama, mahali pa kupumzikia, yaani hekalu la maisha ya kiroho.

Huu ndio unaopaswa kuwa ni mwelekeo wa maisha ya kiroho kwa waamini, daima kutembea kuelekea kwenye nchi ya ahadi. Huu ndio mwanzo wa maishaya familia ya Kikristo! Anasema Baba Mtakatifu Francisko! Mkristo anapaswa kuwa ni chemchemi ya baraka ya Mungu kwa waja wake, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini. Waamini wanapaswa kupeana baraka, kwa kuwatakia wengine mema, ili kwenda kinyume na mwelekeo wa wengi, ambao hawawatakii jirani zao mema katika maisha. Ulimi uwe mwepesi kubariki badala ya kutangaza mabaya ya wengine. Waamini wanapaswa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kutumainia ahadi zake, ili kweli waweze kuwa ni chemchemi ya baraka kwa wengine!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.