2017-06-26 09:53:00

Rais Paul Kagame wa Rwanda ajitosa kuwania Urais awamu ya tatu!


Jukumu la kulinda uhuru na haki msingi za binadamu uko mikononi mwa dola ambayo ina vyombo vyake kama: Mahakama na Bunge. Haki msingi za binadamu zimeendelea kukua na kupanuka kwa kuzingatia haki za kiraia na kisiasa; haki za kiuchumi, kijamii na kitamaduni; haki za pamoja, haki za watu na haki za makundi. Utekelezaji wa haki msingi za binadamu unakwenda sanjari na uwepo wa haki na wajibu katika jamii.

Bara la Afrika, kwa sasa linakabiliana na changamoto ya utawala bora unaojulikana kama utawala wa sheria: kwa kuzingatia sheria,  kanuni pamoja na haki msingi za binadamu. Utawala bora unazingatia ukweli na uwazi; uwajibikaji na demokrasia, yaani: utawala wa watu. Hapa jambo la msingi linalopewa kipaumbele cha pekee ni uwepo wa uhuru na uhalali katika kuendesha chaguzi, kupokea maoni, kuondokana na tabia ya ulimbikizaji wa madaraka kwa mtu au kikundi cha watu wachache ndani ya jamii; matumizi mabaya ya madaraka pamoja na uwepo na wawakilishi wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kimsingi, Bara la Afrika linahitaji viongozi bora watakaosimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Uongozi si kichaka cha watu kutaka kujinufaisha wao binafsi. Bali uongozi ni fursa makini ya kusikiliza watu, kuwaonesha watu njia na dira ya kupata mafanikio katika maisha kwa kupambana kufa na kupona na ujinga, umaskini na baa la njaa. Uongozi ni ushuhuda unaofumbatwa katika ukweli na uwazi; uaminifu na uadilifu. Nchi mbali mbali Barani Afrika ziko kwenye maandalizi ya chaguzi kuu, ili kuwapata viongozi watakaosimamia utawala bora, ili kweli Afrika iweze kucharuka na kuondokana na viongozi wanaotafuta madaraka kwa ajili ya mafao yao binafsi!

Rais Paul Kagame wa Rwanda amekubali kwa mara ya tatu kupokea dhamana ya kuwania tena kugombania uongozi kama Rais wa Rwanda, akichuana na wengine kama Frank Habineza anayeonesha upinzani mkali kwa Rais Kagame. Rwanda anasema Rais Kagame, imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya saratani ya rushwa; imeendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao pamoja na kucharuka kwa maendeleo endelevu ya wananchi wengi wa Rwanda, hali inayojionesha katika maboresho ya sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii.

Rais Kagame anayehesabiwa kuwa ni “Baba wa Rwanda Mpya” iliyoibuliwa baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, wakati mwingine, amekuwa akishutumiwa na wapinzani kwamba, anaingilia uhuru wa vyombo vya habari, ili kuwakata kauli wapinzani! Ikumbukwe kwamba haki zinazotanua wigo wa demokrasia na usawa wa binadamu nu muhimu sana kwa mustakabali wa nchi husika. Hizi ni pamoja na haki za kushiriki katika utawala wa nchi, uhuru wa kujieleza na kutoa maoni. Hizi ni haki za kupiga na kupigiwa kura wakati wa chaguzi. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya viongozi wengi wa Bara la Afrika ni kutaka kupindisha katiba, ili waendelee kubaki madarakani, hali ambayo imepelekea machafuko ya kisiasa na matumzi ya nguvu kupita kiasi katika baadhi ya nchi za Kiafrika! Ni matumaini ya familia ya Mungu Barani Afrika kwamba, chaguzi zilizoko katika nchi mbali mbali Barani Afrika zitafanyika kwa kuzingatia ukweli, uhuru, uwazi, amani na umoja wa kitaifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.