2017-06-24 13:54:00

Utamaduni wa kifo ushindwe kwa ushuhuda wa Uwepo wa Kristo mfufuka


Mmezaliwa kushuhudia kwamba Ufufuko wa Kristo ni msingi wa maisha ya kikristo, ili mtangaze umuhimu wa ufufuko binafsi, na kusimamia jumuiya katika utume wake wa kuhudumia na kujenga ufalme wa Mungu. Kwa namna ya pekee, akiigusa mioyo ya waliohudhuria, Baba Mtakatifu Francisko siku ya Ijumaa, tarehe 23 Juni 2017, katika Hotuba yake kwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa Shirika la Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo, uliokuwa ukiongozwa na tema, Mashahidi wa Uwepo wa Bwana Mfufuka, kutoka kwenye jumuiya kuelekea duniani, amewaalika kuishi kwa kina karama yao.

Ndugu wa Shirika la Ufufuko wanashuhudia Uwepo wa Kristo mfufuka kwa namna ya Maria Magdalena, mtume wa mitume. Maria Magdalena anamtafuta Kristo kati ya wafu, lakini anampata akiwa hai. Ujasiri wa Maria Magdalena na wenzake, kutoka alfajiri na mapema kwenda kumtafuta Bwana, uwe ujasiri wa ndugu wa Ufufuko kutoka kwenye jumuiya zao na kwenda kumtafuta Bwana mfufuka, sio kati ya wafu, bali mahali alipo, kwenye utume kila kona ya dunia ambapo wanahudumia.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watangaze habari njema, ya kile ambacho wao wanakiona hata kama wengi hawakioni, yaani Uwepo wa Bwana mfufuka kwenye maisha ya kila siku. Kwa ushuhuda wao, waamini wapate kutambua kwamba sio wakati wa kuishi kwenye huzuni na ukiwa, bali waishi katika furaha ya Uwepo wa Kristo mfufuka. Ndugu wa Ufufuko wanaalikwa kumruhusu Kristo mfufuka akutane nao kila siku katika njia zenye kukatisha tamaa na kwenye changamoto za shughuli zao kama wanafunzi wa Emmaus. Kukutana kwao na Kristo mfufuka ndiko kutawapa nguvu na furaha ya kukimbia ili kutoka kwenye jumuiya zao na kwenda duniani kuutangaza Uwepo wa Bwana mfufuka.

Wengi leo ingawa wanafahamu kuwa Kristo kafufuka kweli, hawana ujasiri wa kutangaza habari hiyo njema ya Uwepo wa Kristo mfufuka kati watu. Ni mwaliko wa kuwatazama wanadamu wote kuwa ni ndugu, kama zawadi ya Mungu, wenye heshima na utu sawa, wanaopaswa kupokelewa na kukirimiwa, hasa wanyonge na wahitaji, kwani ni kati yao ndipo waaamini wanakutana na Kristo mfufuka. Changamoto zitakuwepo kila wakati, hivyo Baba Mtakatifu Francisko anawaalika ndugu wa Shirika la Ufufuko kuishi kidugu katika jumuiya na kusaidiana katika hija ya maisha wakichuchumilia utakatifu kwa pamoja.

Kristo amewazawadia wafuasi wake furaha ya ndani na mwanga wa fumbo la Pasaka. Furaha ya ndani inayowawezesha kumfahamu Kristo na mapenzi yake, jambo linalowasukuma katika utume. Mwanga wa fumbo la Pasaka unawarudishia matumaini thabiti, kama anavyofundisha Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwenye Barua yake ya Kitume Spe salvi, Tumaini linalookoa, kwamba, waamini wanafufuliwa ili wafufue wengine, wanakombolewa ili wakombowe wengine, wanawekwa huru ili wawaweke huru wengine, wanazaliwa upya ili wawape uzima upya wengine wanaokutana nao katika maisha ya kila siku.

Jamii ya leo inaendekeza maisha ya huzuni na utamaduni wa kifo, Baba Mtakatifu Francisko anasisitiza kushinda utamaduni wa kifo na kutangaza maisha ya ufufuko ndani ya Kristo. Mwaliko kwa kila mwamini kuingia ndani ya kaburi lake binafsi, kusukuma mawe yanayomzuia kuishi uzima, na kuwa jasiri wa kutoka ndani ya kaburi hilo kwa furaha. Baba Mtakatifu Francisko anawaasa ndugu wa Shirika la Ufufuko kukumbuka yaliyopita kwenye karama yao kama chemchemi ya maji ya uhai na sio maji yaliyofungwa kwenye chupa. Wakumbatie maisha ya sasa kwa mapendo hai kwa Kristo, na wawe na matumaini ya mbeleni kwa kutambua kuwa ni Kristo ndiye anayeongoza hatua za utume wao siku hadi siku.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.