2017-06-24 09:32:00

Simamieni haki msingi za binadamu nchini DRC!


Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, inakabiliwa na hali ngumu sana ya maisha kutokana na vita ya muda mrefu ambayo imepelekea pia kuvunjwa kwa haki msingi za binadamu! Waathirika wa kuu ni wananchi wasiokuwa na hatia na kwamba, hata taasisi za kidini nazo zimeanza kuathirika vibaya sana kutokana na kuharibiwa kwa miundo mbinu ya ibada, hasa Mkoani Kasai, ambako hivi karibuni kumetokea mauaji makubwa ya raia wasiokuwa na hatia!

Haya ni matokeo ya kinzani na mipasuko ya kisiasa ambayo hayakupewa uzito wa juu na Jumuiya ya Kimataifa, licha ya juhudi za kuanzisha mchakato wa haki, amani na upatanisho, ambao bado unaendelea kusua sua hadi sasa! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, nchini Uswiss, wakati wa kujadili kuhusu msaada wa kiufundi na jinsi ya kuwajengea wananchi wa DRC uwezo katika kukabiliana na changamoto za maisha. Mkutano huu umefanyika, tarehe 21 Juni 2017.

Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, Serikali ya DRC itaonesha ushirikiano mkubwa na wadau mbali mbali ili kuhakikisha kwamba, vita na ghasia nchini humo vinasitishwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na upigwaji rufuku wa biashara ya silaha nchini DRC, biashara ambayo imeendelea kupandikiza mbegu ya chuki na utamaduni wa kifo! Dhamana ya kulinda raia na mali zao ipewe msukumo wa pekee, tayari kuanza kujikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano miongoni mwa wananchi wa DRC. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kuwa na wapatanishi ambao watasaidia kuyakutanisha makundi yanayopingana na kusigana nchini DRC.

Jumuiya ya Kimataifa anasema Askofu mkuu Ivan Jurkovič, haina budi kuhakikisha kwamba, inatengeneza mazingira yatakayowawezesha wakimbizi kutoka mkoani Kasai, DRC, kuweza kurejea tena katika makazi yao. Lakini, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinalindwa, zinadumishwa na kuendelezwa nchini DRC na kwamba, haikubaliki tena watoto kuchukuliwa na kupelekewa mstari wa mbele kama chambo cha mapigano, badala ya kupewa nafasi ya kuendelea na masomo darasani. Baba Mtakatifu anasema, umefika wakati, kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na dhamiri nyofu, itakayowasukuma na kuwaongoza kusimama kidete kulinda na kuwatetea watoto wanaopelekwa mstari  wa mbele kama chambo cha vita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.