2017-06-24 16:23:00

Salam na matashi mema kwa waamini wa dini ya Kiislam!


Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kilikuwa ni kipindi cha swala, sadaka na kufunga! Kardinali Angelo Scola, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Milano, Italia anaungana na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini kuwatakia waamini wa dini ya Kiislam salam na matashi mema, amani na utulivu baada ya kuhitimisha kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mkutufu wa Ramadhani. Kardinali scola anakazia kwa namna ya pekee kabisa umuhumu wa waamini wa dini mbali mbali kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana; daima wakijitahidi kuwatanguliza jirani zao, huku wakiwa na bidii zaidi katika maisha ya kiroho!

Waamini wanahimizwa na Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na upendo kutafuta na kukuza kile kilicho chema katika maisha ya jirani zao, ili kiweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani umoja, upendo na udugu. Kardinali Scola anakaza kusema, Mfungo wa Mwezi Mkutukufu wa Ramadhani umewakirimia waamini wa dini ya Kiislam, matunda ya maisha ya kiroho ambayo wanapaswa kuyaendeleza hata baada ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Mshikamano wa umoja na upendo, uwe ni faraja kwa watu wanaoteseka kutokana na vita, ghasia, njaa, uchafuzi wa mazingira sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Huu ni mshikamano unaopaswa kujengwa na wale wanaojisikia pweke na kusahauliwa na jamii zao. Hawa ndio wakimbizi na wahamiaji, wanaohitaji msaada na faraja, ulinzi, usalama na haki zao msingi kulindwa na kudumishwa. Hawa ni watu waliokata tamaa ya maisha, wanaopaswa kuonjesha Injili ya matumaini, ili hatimaye, kukuza na kudumisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu. Familia ya Mungu Jimbo kuu la Milano, inapenda kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, ili kwa pamoja waweze kuzima kiu ya maisha, ukweli, wema na uzuri, mambo ambayo yameshuhudiwa na vijana wengi huko Milano.

Miaka 50 iliyopita, yaani kunako mwaka 1967 Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini liliundwa na tarehe 19 Mei 1964 Mwenyeheri Paulo VI akatuma ujumbe wa kwanza wa salam na matashi mema kwa waamini wa dini ya Kiislam  wakati wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Tangu wakati huo, viongozi mbali mbali wa Kanisa wameendelea kutuma ujumbe wa matashi mema kwa waamini a dini ya Kiislam wakati wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kunako mwaka 1991 Mtakatifu Yohane Paulo II alikazia umuhimu wa amani na kunako mwaka 2013, Papa Francisko alipokuwa anaanza maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro aliwaandikia ujumbe akikazia umuhimu wa waamini kuheshimiana na kuthaminiana kwa njia ya elimu.

Katika kipindi cha miaka hamsini tangu kuanzishwa kwake, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini limekuwa likijizatiti siku hadi siku kwa ajili ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali. Baraza linatekeleza dhamana na majukumu yake kwa kusaidiwa na Makanisa Mahalia sehemu mbali mbali za dunia pamoja na Mabalozi wa Vatican. Ujumbe huu, umesaidia kukuza na kudumisha mahusiano mema kati ya Wakristo na Waislam, kwa kuendeleza urafiki na ujirani mwema pamoja na kushughulikia changamoto mamboleo kwa pamoja.

Ujumbe wa mwaka huu kwa namna ya pekee, unajikita katika Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni ujumbe unaotolewa kwa watu wote wenye mapenzi mema. Baba Mtakatifu Francisko anaialika familia ya Mungu duniani kubadili, maamuzi na  mtindo wa maisha unaopelekea uharibifu mkubwa wa mazingira kwa wao wenyewe pamoja na watu wengine duniani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna baadhi ya falsafa, maisha ya kidini na kitamaduni yanayohatarisha uhusiano mwema kati ya binadamu na mazingira.

Jambo la msingi ni kutambua kwamba, dunia ni nyumba ya wote inayotumiwa na familia yote ya Mungu, kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na mwelewa mpana zaidi kuhusu mazingira bila kuangalia imani au itikadi ya mtu awaye yote! Hii inatokana na ukweli kwamba, uharibifu wa mazingira ni janga kwa binadamu wote, kumbe, linahitaji watu kufanya toba na wongofu wa ndani unaofumbatwa katika elimu, uwazi wa maisha ya kiroho sanjari na kuwa na wongofu wa kiekolojia duniani unaodhibiti kwa kiasi kikubwa changamoto hii mamboleo.

Uhusiano wa waamini na Mwenyezi Mungu unapaswa kuboreshwa zaidi kwa kujikita katika utunzaji bora wa mazingira na mahusiano mema kati ya binadamu kwa kutambua kwamba, dhamana na kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora ni sehemu ya muhimu sana kwa waamini wa dini zote. Ujumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini kwa ajili ya kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umetiwa sahihi na Kardinali Jean Lous Tauran na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot kwa kuwatakia waamini wote wa dini ya Kiislam, mfungo mwema unaojikita katika: kufunga, kuswali na kutenda matendo mema na hatimaye, wanawatakia utulivu, furaha na ustawi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.