2017-06-24 08:46:00

Maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano yalisaidie Kanisa kuinjilisha!


Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya “Inter Mirifica” yaani “Njia za Mawasiliano ya Jamii” wanakazia umuhimu wa mawasiliano ya jamii unaoweza kumsaidia au kumwangamiza mwanadamu, pale ambapo kanuni maadili, utu wema, ustawi na maendeleo ya wengi havitazingatiwa. Vyombo vya mawasiliano ya jamii havina budi kusaidia kutangaza na kushuhudia ukweli; kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya watu; kukuza na kuendeleza uhuru unaowawajibisha watu kimaadili sanjari na kusaidia mchakato wa watu kupyaisha maisha yao ya kiroho na kiutu! Kimsingi njia za mawasiliano ya jamii hazina budi kuhakikisha kwamba, zinasaidia kutoa huduma makini ya mawasiliano katika medani mbali mbali za mawasiliano ya kijamii ili kudumisha umoja, mshikamano na udugu.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walitaka Kanisa kuhakikisha kwamba, linatumia maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Njia za mawasiliano zisaidie katika shughuli mbali  mbali za kichungaji zinazofanywa na kutekelezwa na Mama Kanisa. Mawasiliano ya Jamii ni sekta ambayo inakua na kupanuka kwa haraka sana, kiasi cha kubeba changamoto, matatizo na fursa ambazo, zinaweza kuvaliwa njuga na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Duniani, inayoadhimishwa kila Mwaka, wakati wa Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni.

Kwa bahati mbaya, hii ni siku ambayo imeachwa wazi kwa ajili ya Makanisa mahalia kuchagua siku ambayo inafaa zaidi. Pengine, umefika wakati kwa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican kuiangalia changamoto hii ili kuweza kuifanyia maboresho makubwa ili Kanisa liweze kutumia kikamilifu maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ufanisi zaidi; kwa kukuza ukomavu na kujenga umoja kati ya watu, daima Mafundisho Jamii ya Kanisa yakipewa kipaumbele cha kwanza. Lengo ni kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya kwa kujikita katika imani, ukweli, upendo na mshikamano katika ulimwengu huu wa digitali. Kipaumbele cha mawasiliano ndani ya Kanisa ni ukweli ambao ni Kristo mwenyewe ambaye ni njia, ukweli na uzima!

Hivi karibuni, Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican, alishiriki katika majiundo endelevu awamu ya IX ya “Summer School” yaliyoandaliwa na Taasisi ya Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya Vyama vya Wafanyakazi Wakatoliki, kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” cha Milano, nchini Italia. Kauli mbiu ya majiundo haya ilikuwa ni “Kanisa na Mawasiliano. Tangu Inter Mirifica hadi kwa Papa Francisko”. Hii mada ilipembuliwa kwa kina na mapana na Monsinyo Dario Edoardo Viganò aliyefafanua kuhusu mageuzi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii ambayo yameleta mabadiliko makubwa hata katika maisha na mahusiano ya watu ndani ya jamii. Kanisa nalo kwa upande wake, limekuwa llikifuatilia mchakato huu hatua kwa hatua katika maisha na utume wake, ili kuliwezesha  kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kati ya watu wa Mataifa.

Tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa limeendelea kujikita katika matumizi ya sayansi na teknolojia ya habari mintarafu Hati ya “Inter Mirifica” yaani “Njia za Mawasiliano ya Jamii”. Kulikuwepo na idadi kubwa ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, pengine hata bila kuzingatia ubora na uwezo wake wa kufikisha ujumbe uliokuwa unakusudiwa. Kwenye Miaka 1960, kwa mfano Kanisa Katoliki nchini Italia, lilikuwa na majumba makubwa ya Sinema yaliyokuwa yanaendeshwa na kusimamiwa na Parokia. Huu pia ni mwanzo wa kuibuka kwa Magazeti yaliyokuwa yanamilikiwa na kuendeshwa na Kanisa

Miaka ya 1980 ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa vitivo vya sayansi ya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya kuwaandaa wataalam katika uwanja wa mawasiliano ya jamii. Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesiani, Chuo Kikuu cha Kipapa cha “Santa Croce” Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian vikawa ni mwanzo wa Kanisa katika kuwaandaa watalaam katika masuala ya sayansi ya mawasiliano ya jamii anasema Monsinyo Dario Edoardo Viganò. Kunako Mwaka 1983, Vatican ikaanzisha Kituo cha Televisheni, CTV ambacho kinaendelea kutoa huduma kwa matukio mbali mbali yanayofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ndani na nje ya Vatican. Kunako mwaka 1998, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, likabuni na kuanzisha Mradi wa Televisheni uliojulikana kama Sat2000, Kituo ambacho kwa sasa kinajulikana kama Tv2000. Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, yaliibua changamoto kubwa katika masuala ya mawasiliano ya jamii. Lakini, ikumbukwe  kwamba, watu wenyewe ni sehemu ya mawasiliano.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kunako mwaka 2015 amethubutu kufanya marekebisho makubwa katika vyombo vya mawasiliano vinavyoendeshwa na kusimamiwa na Vatican na kuviweka chini ya usimamizi na uratibu wa  Sekretarieti ya Mawasiliano ya Jamii mjini Vatican ambayo kimsingi inaunganisha: Radio Vatican, Gazeti la L’Osservatore Romano na Kituo cha Televisheni cha Vatican, yaani, CTV. Lengo ni kuunganisha nguvu za Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji mpya katika ulimwengu wa digitali unaotoa fursa kwa watu kuweza kupata habari kwa ukamilifu zaidi, huku sauti, picha na maandishi yakiunganishwa yote katika chombo kimoja cha mawasiliano. Hii ni ni fursa ya kutumia vyema rasilimali watu, fedha na teknolojia ili kusoma alama za nyakati, tayari kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa mawasiliano ya jamii. Sekretarieti ya Mawasiliano ya Jamii mjini Vatican inapania kushirikiana kwa karibu zaidi na Makanisa mahalia katika mchakato mzima wa mawasiliano ya jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotishwa viongozi, wafanyakazi na wadau mbali mbali wa vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyoongozwa na kusimamiwa na Vatican kujipanga upya ili kuweza kupata ufanisi zaidi kwa gharama nafuu, kwani mawasiliano ya jamii ni sekta inayohitaji uwekezaji endelevu kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kila wakati! Baba Mtakatifu Francisko hata katika umri wake, ambao wengi wangedhani kwamba, ni mtu wa “P.O. BOX” lakini ameendelea kujikita katika matumizi ya mitandao ya jamii, hali inayomwezesha kuwafikia watu wengi zaidi katika maisha yao ya kawaida!

Itakumbukwa kwamba, ni kati ya viongozi wa Kanisa, ambao wamekuwa na mvuto mkubwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii ndani na nje ya Kanisa; kwa waamini na wale wasioamini kutokana na mtindo wake wa maisha unaowashangaza na kuwagusa watu wengi. Ni kiongozi anayetumia lugha rahisi inayokita ujumbe wake moja kwa moja katika masikio, akili na nyoyo za watu! Hii ni kutokana na mantiki kwamba, Injili ya Kristo ni Habari Njema kwa wote pasi na ubaguzi wala tabia ya kutaka kumtenga mtu! Ni kiongozi anayependa kutekeleza kile anachokisema kama ushuhuda wa imani tendaji! Kwa njia hii, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni jirani kwa watu wengi duniani.

Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican anakaza kusema, tatizo, changamoto na fursa ya Kanisa si teknolojia ya mawasiliano ya jamii; maudhui yanayokusudiwa, bali ni kuhakikisha kwamba, sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii inasaidia kudumisha mchakato wa uinjilishaji mpya unaowakutanisha watu na tamaduni mbali mbali. Hapa kuna haja ya kuwa na lugha makini, mifumo sahihi na nyenzo makini zinazoweza kuwafikia watu mbali mbali mahali walipo katika ulimwengu wa digitali. Lengo ni kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia! Huu ni wakati wa kusikiliza kwa makini bila ya kuwa na maamuzi mbele pamoja na kujifunza kutoka kwa wengine, changamoto iliyovaliwa njuga na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ushuhuda wa waamini ni njia makini ya mawasiliano yenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.