2017-06-23 09:35:00

Mwanadamu ameumbwa mwili na roho!


Miaka ya mwanzo ya Kanisa imetupatia mfano wa mashahidi wengi ambao wamejitoa mhanga na kufa kwa kumwaga damu zao kwa sababu ya kuisimamia imara imani yao. Matukio hayo yamekuwa ni fahari na kichocheo cha kuimarisha imani ya kikristo na pia kuupatia ukristo nguvu katika jamii ya wanadamu. Mashahidi wa imani waliifikia hali hiyo kwa utayari wao wa kuthubutu na kukubali kuisimamia ukweli ambao wameupokea. Jamii ya wakati wao haikuwa tayari kuupokea ukweli wa Kristo, ukweli ambao ulinuia kumkomboa mwanadamu na kumpatia hadhi yake stahiki. Je, mazingira hayo ya upinzani hayapo leo? Je, Ujumbe wa Kristo umekubalika? Ni wazi upinzani huo upo na unatudai ushahidi mithili ya mashahidi wa kipindi hiko cha awali cha Kanisa.

Injili ya Dominika ya leo inatuelezea ukweli juu ya mwanadamu, ukweli ambao unapaswa kusimamiwa. Mwanadamu ni mpendwa na kitu cha thamani mbele ya Mungu. Thamani yetu inajifunua katika ukweli wetu kihalisia, kwamba tumeumbwa mwili na roho. Mwenyezi Mungu anatuthamini katika ukweli huo na kututunza katika ukweli huo. Lakini ukweli jamii yetu leo hii hauijali hadhi hii ya kibinadamu; mwanadamu anatambulika na kuthaminika zaidi katika mwili. Yale yanayoonekana, yale yanayoshikika, yale tunayoweza kuyaonja ndiyo tunayapigania kwa nguvu zote. Ndiyo maana wengi tunaogopa wanaouua mwili na si wale wanaoiua roho. Tunapambana kuilinda miili yetu na siyo vyote kwa pamoja yaani mwili na roho. Kristo anatuonya akituambia kwamba: “mwogopeni Yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanamu”.

Onyo hilo la Kristo ni kutugutusha na kututaadharisha kutunza miili yetu na roho zetu pamoja. Dhambi ya mwanadamu ambayo ni matunda ya kutawaliwa na shetani ndiyo hutufikisha katika kifo cha mwili na roho. Mwanadamu anayepoteza uhai wa kiroho kwa sababu ya dhambi hudanganyika na mafanikio ya kimwili au kijamii yanayoonekana lakini mwishoni husononeshwa na ufupi wa mafanikio hayo. Wangapi hupenda kujidanganya wapo safi au wapo sawa nje nje tu lakini ndani wameoza? Yanapogundulika ya ndani hubaki katika hali ya masikitiko na kukata tamaa. “Hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa”. Roho iliyokufa, yaani yeye atendaye si sawa na mapenzi ya Mungu, yeye ambaye ametengana na Mungu akidhani kwamba si sehemu ya maisha yake  na hivyo kuamua kutenda atakavyo mwishoni atafunuliwa na kuoneshwa anguko lake.

Mwenyezi Mungu anatupenda, anatuthamini na kuutunza uhai wetu kimwili na kiroho. Kama vile tunavyoshuhudia akiwatunza viumbe mbalimbali kwa mahitaji yao ya kila siku tupate uhakika kwamba “sisi ni bora kuliko mashomoro wengi”. Imani yetu thabiti kwake na kujitegemeza kwake ndiko kunakotuhakikishia uwepo wa ulinzi na upendo wake kwetu. Imani hiyo huonekana katika muunganiko wetu nae kwa njia ya Kristo anayetuambia kwamba: atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele ya Baba yangu aliye mbinguni. Bali yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni”. Huo ndiyo mwaliko wa ushuhuda wa imani yetu kwa Mungu ili tuunganike naye daima.

Ujasiri wa Wakristo wa kwanza wa kuutunza ukweli ulikuwa ni ushuhuda wao wa kuunganika na Mwenyezi Mungu na ni kielelezo kwetu cha kusimama imara katika ukweli na haki. Jamii yetu ya leo inaendelea kutoa mazingira kinzani kwa ushuhuda wa kiimani. Mfano wa mateso na Nabii Yeremia, tunaoyaona katika somo la kwanza yanajitokeza katika namna mbalimbali. Tunaendelea kusikia vitisho vingi dhidi ya watu wema: “mshitaki, nasi tutamshitaki, huenda akahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake”. Kelele hizi kidunia hunuia kututoa katika ukweli na kujirandanisha na uovu wa kidunia. Maneno ya kashfa na ajali nyingi za kusukwa huandamana na watu hawa. Katika jamii yetu ya leo ya maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano tumeshuhudia watu wengi wema wanachafuliwa hadhi zao kwa kutaka tu kunyamazishwa na uovu uendelee.

Hii ni hali ambayo inatudai kufanya ushuhuda wa kiimani. Ushuhuda wa leo unaweza kuwa si wa kumwaga damu lakini tunaweza kuubatiza na kuuita “ushuhuda wa kumwaga damu nyeupe”.  Njia pekee ya kufikia hapo ni kujivika Kristo katika maisha yetu. Mtume Paulo anamtaja kama sababu ya kuindoa dhambi ulimwenguni. Neno la Mungu linatuambia: “Kwa maana ikiwa kwa kukosa kwake yule mmoja (Adamu) wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu, na kipawa kilicho katika neema yake mwanadamu mmoja Yesu Kristo kimezidi kwa ajili ya wale wengi”. Neema hiyo tuipatayo kwa njia ya Kristo ni sababu ya ujasiri wetu wa kuutetea ukweli na kutovutika na malimwengu. Sisi wanadamu tunapotenda katika Kristo tunatenda katika ukweli wote na hivyo kuitambua na kuithamini hadhi yetu ya kibinadamu, yaani kutunza roho zetu na miili yetu katika ukamilifu.

Utamu wa maendeleo ya kidunia, hamu ya ufahari wa mali na madaraka hutuhadaa sana hata tunashindwa kusimamia ukweli katika maisha yetu. Yapo majanga mengi ya kibinadamu, mathalani biashara za madawa ya kulevya, ukahaba, rushwa, unyonyaji na mengineyo mengi ambayo chanzo chake ni kukosa ujasiri kuwa mashuhuda wa ukweli kwa ulimwengu. Viongozi wengi wa kijamii au wale wenye nafasi mbalimbali za kuistawisha jamii ya kibinadamu hutuhadaa kwa maneno matamu matamu ya nje ili wakubalike na jamii lakini ndani mwao wamejaa hila. Hawaingiwi na woga hata kidogo kuharibu roho zao kwa matendo ya dhambi, ili mradi tu mambo yao ya kidunia yanasonga mbele. Wanaogopa kufedheheshwa mithili ya Nabii Yeremia na hivyo mara nyingi wanabaki katika mtindo wa “funika kombe mwanaharamu apite”. Yote haya ni changamoto kwetu sisi Wakristo na tunavyozidi kushuhudia uovu zidi ya ubinadamu ni mashitaka kwetu kwamba tumeshindwa kuwa mashuhuda wa ukweli.

Tujivike ujasiri huo na kuuthamini utu wetu katika ukamilifu wake. Daima tujikumbushe ukweli juu ya mwanadamu kwamba ni mwili na roho na hivyo kufanya bidii ya kustawisha vyote. Tutambue kwamba roho iliyo katika kweli, iliyojazwa upendo wa kimungu na inayojiunganisha na Mungu daima ni injini madhubuti ya kuustawisha mwili na kuufanya kuionja furaha ya kweli na yenye kudumu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.