2017-06-22 17:52:00

Rais Magufuli apongezwa kwa kuonesha uchungu kwa rasilimali za nchi!


Mheshimiwa Olusegun Obasanjo, Rais mstaafu wa Nigeria amempongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuonesha mfano bora katika Bara la Afrika katika kusimamia uchumi na kutetea maslahi ya nchi katika uwekezaji. Rais mstaafu Obasanjo ametoa pongezi hizo siku ya Jumanne, tarehe 20 Juni, 2017 muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam. Rais mstaafu Obasanjo amesifu juhudi za Rais Magufuli kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali duniani na kusimamia ipasavyo sera ya kuhakikisha nchi inanufaika, badala ya kuacha wawekezaji wakijinufaisha wenyewe na nchi kuambulia kiasi kidogo cha mapato.

Rais mtaafu Obasanjo amepita nchi nyingine pia kama Msumbiji na Malawi akisisitizia masuala ya uchumi na namna nchi za Afrika zinavyopaswa kunufaika na uwekezaji katika nyanja mbalimbali na sio kuwanufaisha wawekezaji, hali nchi inabaki na kitu kidogo sana. Katika hili, Rais Magufuli ameonesha mfano mzuri sana kwa viongozi wa Afrika, amesema Rais mstaafu Obasanjo. Taarifa hizi zimetolewa na Bwana Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, jijini Dar es salaam.

Wakati huo huo, Bwana Kassim Majaliwa, Waziri mkuu wa Tanzania amewaasa waamini wa dini za kiislamu na kikristo wahakikishe nyumba zao za ibada hazitumiki kuleta migogoro bali kumwabudu Mungu. Kayasema hayo siku ya jumatano, tarehe 21 Juni 2017, wakati wa ibada ya futari wilayani Chato, mkoani Geita, akimwakilisha Rais John Magufuli, ambaye hakuweza kufika sababu ya kutingwa na majukumu mengi ikiwa ni pamoja na kukutana na wageni wa kimataifa.

Ibada hiyo ya futari wilayani Chato ilihudhuliwa na mamia ya waamini na viongozi wa dini za kikristo na kiisalmu. Waziri mkuu Majaliwa amesisitiza kwamba, serikali ya Rais Magufuli itaendelea kuheshimu dini zote, lakini haitofurahishwa na habari za kusikia msikitini wamechalazana viboko kugombania uongozi au kanisa Fulani wamepigana kugombea mchungaji. Amekumbusha kwamba Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa toba kwa waamini wa dini ya kiislamu. Ni mwezi unaofundisha amani, uvumilivu na kusameheana. Hivyo ni muhimu kudumisha utulivu na amani ya nchi. Waziri mkuu Majaliwa kawasihi sana pia waamini wa kiislamu na kikristo kuendelea kumuombea Rais Magufuli na viongozi wengine wa serikali, ili waweze kuamua na kutenda kwa kuongozwa na Mungu.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.