2017-06-22 17:27:00

Papa Francisko ataja sifa za kiongozi bora!


Waamini wanaalikwa na kuhamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zao, bila ya kutaka kujitafutia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko! Wajitahidi kuguswa na mahangaiko, shida za jirani zao pamoja na kuwa na ujasiri wa kuweza kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki zao msingi kama alivyofanya Don Lorenzo Milani. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 22 Juni 2017 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anawakumbusha viongozi wa Kanisa kwamba, mchungaji mwema ni yule anayethubutu kujisadaka bila ya kujibakiza kiasi hata cha kutoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake. Mtakatifu Paulo anajionesha kuwa ni kiongozi na mfano bora wa kuigwa; yuko tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwatetea watu wake na wala si kama mtu wa mshahara ambaye akiona hatari mbele yake anaweza kitimuka na kuwaacha kondoo wakiteketea. Kiongozi bora anapaswa kuwa huruma, kiasi hata cha kuthubutu kuwaambia watu anawaongoza kwamba, anawaonea wivu mtakatifu.

Kiongozi bora ni yule anajitahidi kutafuta mbinu za kung’amua mambo mbali mbali, ili kuboresha huduma za kichungaji, ari na maisha ya kiroho kwa kutambua kwamba, maisha daima yamesheheni vishawishi na kinzani. Ni mtu anayetambua maana ya kupenda kwa dhati, lakini pia anafahamu kwamba, katika upendo kuna changamoto na vikwazo vyake kama ilivyotokea kwa Adamu na Hawa kusalitiwa na nyoka! Kiongozi bora anapaswa kuwa ni mwaminifu kwa maisha na utume wake. Katika historia ya wokovu, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna kurasa zinazowaonesha watu wa Mungu jinsi walivyokosa uaminifu, wakaanza kuabudu miungu wa kigeni na kukengeuka katika maisha ya ndoa na familia! Kiongozi bora anapaswa kuwa na ujasiri wa kukemea maovu ndani ya jamii; kuwa na mang’amuzi ya kutambua wapi ambapo kuna hatari katika maisha, ili aweze kuwaongoza watu wake katika njia ya salama, ukweli na amani. Wazazi wawe na ujasiri wa kuwakemea watoto wao pale wanapoanza kukengeuka na kupotoka katika imani, maadili na utu wema.

Baba Mtakatifu anasema hivi karibuni amefanya hija ya binafsi kutembelea katika makaburi ya Maparoko wawili wa Italia yaani Don Lorenzo Milani na Don Primo Mazzolari ambao katika maisha na utume wao, wameacha mfano bora wa kuigwa na Mapadre wengine katika utakatifu wa maisha na huduma kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Don Lorenzo Milani alijisadaka kuwafundisha watoto wa maskini, ili waweze kupata elimu ambayo ingewaletea ukombozi na wala hakutegemea kulipwa chochote na watoto hawa! Baba Mtakatifu anawataka viongozi wa Kanisa kukazia sifa hizi kwa ajili ya huduma kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.