2017-06-21 16:57:00

Mpasko wa kisiasa Venezuela: Muhimu ni majadiliano: ukweli na uwazi!


Mkutano mkuu wa Umoja wa Nchi za Amerika, ulioanzishwa kunako mwaka 1948 kwa kuziunganisha nchi 35 kwa lengo la kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, umehitimishwa mjini Cancun, Mexico, bila mafanikio kuhusiana na hali tete ya kisiasa, kiuchumi na kijamii huko nchini Venezuela.  Venezuela kwa upande wake, imesikika ikisema, isengeweza kutekeleza maamuzi ambayo yangetolewa na Umoja wa Nchi za Amerika na kwamba, kimsingi tayari Venezuela ilikwisha kujiondoa katika Umoja huu. Pamoja na mambo mengine, wajumbe walikuwa wameiomba Serikali ya Venzuela kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa kama sehemu ya mchakato wa kumaliza machafuko ya kisiasa nchini Venezuela ambayo tayari yamekwisha sababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema, njia pekee ya kuweza kutoka katika machafuko haya ya kisiasa na kuanza kujikita katika misingi ya haki na amani ni majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya watu wengi. Lengo ni kutaka kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli. Mkutano mkuu wa Umoja wa Nchi za Amerika  uliofunguliwa hapo tarehe 19 – 21 Juni 2017 umeshindwa kufikia muafaka kutokana na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa nchi wanachama!

Askofu mkuu Bernardito Auza anasema, tangu mwanzo: Baba Mtakatifu Francisko, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Venezuela kwa nyakati mbali mbali wametoa kipaumbele cha kwanza kwa majadiliano ya kina, katika ukweli na uwazi kwa pande zote zinazohusika kuvuka misimamo yao ya kisiasa na kuanza kusikiliza sauti ya wananchi wa Venezuela, tayari kusimama kidete, kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican imekuwa wazi sana kuhusiana na suala la Venezuela kwa kukazia umuhimu wa kusitisha ghasia, fujo na vurugu na kuanza kuambata ukweli, haki na amani.

Kardinali Pietro Parolin, kunako mwezi Desemba 2017 aliwaandikia barua wadau mbali mbali katika mgogoro wa kisiasa nchini Venezuela; barua hii inaweza kuwa ni rejea na msingi wa majadiliano ya kisiasa nchini Venezuela. Kati ya mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza ni kuanzisha mchakato wa uchaguzi mkuu utakaopaswa kuwa huru na wa haki ili kweli wananchi waweze kuamua kuhusu hatima yao ya maisha. Alipendekeza njia kadhaa za kutekelezwa ili kuhakikisha kwamba, waathirika wa ghasia na mipasuko ya kijamii nchini Venezuela wanapata huduma na msaada unawafikia walengwa.

Ili amani ya kweli iweze kufikiwa kulikuwa na haja pia ya kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa na kwamba, majadiliano ya kisiasa yanapaswa kusimamiwa na Jumuiya ya Kimataifa, kwani ghasia na vurugu za wakati huu ambazo zimeligusa hata Kanisa nchini Venezuela ni hatari kwa mustakabali wa nchi hii kwa siku za usoni anasema Askofu mkuu Bernardito Auza. Uamuzi wa Serikali kuitisha Bunge la dharura si jibu sahihi kutokana na hali tete ilivyo nchini Venezuela, jambo linaloweza kuhatarisha pia demokrasia. Serikali ya Venezuela inapaswa kusikiliza sauti ya wananchi na kuzipatia majibu muafaka changamoto zinazojitokeza. Ni matumaini ya Askofu mkuu Bernardito Auza kwamba, majadiliano ya kisiasa nchini Venezuela yataweza kusimamiwa vyema na Jumuiya ya Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.