2017-06-20 16:31:00

Tanzia: Kardinali Iva Dias amefariki dunia!


Kardinali Ivan Dias, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, na Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Bombay, tarehe 19 Juni 2017 amefariki dunia mjini Roma akiwa na umri wa miaka 81. Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali, Jumatano, tarehe 21 Juni 2017 majira ya saa 9: 00 Alasiri ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Kardinali Dias na Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Maziko, kadiri ya taarifa zilizotolewa na Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa.

Marehemu Kardinali Ivan Dias alizaliwa tarehe 14 Aprili 1936 huko Bombay, India. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 8 Desemba 1958 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kunako mwaka 1964 akaanza utume wake wa Kidiplomasia mjini Vatican. Katika maisha na utume wake, aliwahi kutekeleza dhamana na utume wake katika nchi za Scandinavia, Indonesia, Madagascar, Visiwa vya Rèunion, Comorro, Mauritius. Kunako tarehe 8 Mei 1982 aliteuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu na hatimaye, Balozi wa Vatican nchini Ghana, Togo na Benin. Akawekwa wakfu kunako tarehe 19 Juni 1982. Baadaye alitekeleza dhamana na utume huu huko Korea kati ya Mwaka 1987 hadi mwaka 1991 na Albania kati ya Mwaka 1991 – 1997.

Kunako tarehe 8 Novemba 1996 hadi mwaka 2006 aliteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bombay. Kunako tarehe 21 Februari 2001, akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Kardinali. Kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2011, aliteuliwa kuwa Mwenyeki wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.