2017-06-20 16:48:00

Padre Primo Mazzolari, alikuwa ni Baba wa maskini na waliotelekezwa!


Maparoko ni nguvu ya Kanisa nchini Italia, wakiweka uhai katika utume hasa wa kibaba katika parokia zao, na waamini wengi wananufaika na huduma hiyo. Maneno haya huyasema sana Baba Mtakatifu Francisko, kayarudia tena siku ya Jumanne katika hotuba yake alipokuwa katika hija yake ya kitume huko Bozzolo nchini Italia, kwa heshima ya kumbukumbu ya Padre Primo Mazzolari.

Padre Mazzolari walimuita paroko wa Italia, na Baba Mtakatifu Yohane XXIII alimsalimu kama tarumbeta la Roho Mtakatifu maeneo ya Padana alikokuwa akiishi na kutoa huduma, wakati Baba Mtakatifu Paulo VI aliwahi kusema, Padre Mazzolari alitangulia mbele kwa hatua ndefu sana na mara nyingi wengine walishindwa kuendana na hatua hizo, kitendo kilichomfanya ateseke na aliokuwa akiishi nao waliteseka pia, lakini ni kawaida kwa maisha ya manabii. Padre Mazzolari alipata malezi ya kikristo wakati wa ujana wake hasa malezi yaliyojali haki na usawa katika jamii, ikiwa ni pamoja na huduma kwa wahamiaji. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake anatumia lugha ya picha, yaani mto, shamba na uwanda, kutoa tafakari juu ya maisha na utume wa Padre Mazzolari.

Padre Primo Mazzolari alitoa huduma yake ya kipadre maeneo ambapo kuna mto unaotililika maji, ambao ni ishara ya ukuu, uweza na neema za Mungu zinazobubujika kuelekea maisha ya wanadamu. Tafakari na mafundisho ya Padre Mazzolari yalikuwa wazi na yenye kueleweka yakiwa yamejikita kwenye utajiri wa Neno la  Mungu. Katika mtililiko wa maisha ya watu, kama mtililiko wa maji ya mto palipo na changamoto nyingi, padre huyu hakurudi nyuma, bali alijifunza kuupokea ukweli na kuishi upendo na ukarimu.

Akiwahubiria waseminari aliwahi kusema kwamba kurudia kusema vitu ni sehemu ya nguvu ya mwanadamu. Hapa Baba Mtakatifu Francisko anasema, kurudia huku alikokuzungumzia Padre Mazzolari, sio ufu wa mawazo, bali ni kurudia kunakoweka ubunifu na imani binafsi kuonesha uhai wa Neno la Mungu, na kwamba anayenena anaamini kweli juu ya hicho anachokisema. Unabii wa padre huyu ulijidhihirisha kwenye kupenda watu na kupenda changamoto za wakati wake huku akimwilisha huruma ya Mungu kati ya watu. Kumbe padre huyu hakuwa analilalamikia Kanisa na watumishi waliomtangulia, bali alikuwa anafanya juhudi za kuboresha hali ya utume wa Kanisa, hivyo alisisitiza sana kufanya utafiti wa dhamiri kwa waamini.

Maisha ya shamba kwa wakati wa Padre Mazzolari yalikuwa ni ya familia ndani ya familia nyingi, yaani maisha ya jumuiya pana ambazo ziliishi katika maeneo ya shamba zikisaidiana kidugu na mshikamano hata katika nyakati za shida na ukosekanaji wa haki. Wengi walikuwa wanajikuta na hamu ya kukimbilia mijini, Padre Mazzolari akawa anapendekeza kutoka katika nyumba za mapadri na nyumba za waamini ili kwenda kukutana na watu katika maisha na shguhuli zao za kila siku, kwani ingawa sio changamoto za kiroho, bado ni changamoto za wanadamu ambazo zinawagusa wote. Kwa namna hii alitambulikana kama paroko wa walio mbali, kwani alihangaikia zaidi walioonekana watu duni na wa kusahauliwa.

Maisha katika uwanda unaofunguka bila mipaka ya usalama, ni mwito wa kurudi kwenye hotuba ya Kristo mlimani kuhusu heri nane. Mwaliko wa ukarimu wa kichungaji kuhangaikia wanyonge na pengine wanaoonewa. Katika jamii ya sasa kuna changamoto za wakimbizi, wahamiaji, ugaidi, myumbo wa demokrasia, umaskini na mambo kama hayo, ambayo yanamtesa sana mwanadamu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wote, na kwa namna ya pekee makasisi, kujitosa katika kukabiliana na changamoto hizi na kuwahudumia wanyonge zaidi.

Padre Mazzolari hakuishi maisha ya anasa, kwani hata kile kidogo alichopata alikitoa kwa wahitaji. Namna ya Mungu ya utendaji, ukiwa na kidogo utahudumia wengi. Hata hivyo inategemea na namna ya mwono wa mtu kama alivyopenda kusema Padre Mazzolari kwamba, ukiwa na ukarimu mdogo utaona wahitaji wachache, ukiwa na ukarimu mwingi utaona wahitaji wengi, na ukiwa huna kabisa ukarimu, hutaona mhitaji hata mmoja. Ukarimu ni shairi la mbinguni lililomwilishwa duniani.

Baba Mtakatifu kawaalika makasisi kukumbuka mwaliko wa kuwa wachungaji wema, kila wakati watangulie ili kuonesha njia kwa waamini. Katika huduma za uinjlishaji Baba Mtakatifu anatahadharisha hatari tatu. Kwanza ni kupinga kila jambo, pili ni shughuli nyingi bila kujali mahusiano mazuri na watu, na tatu ni kushughulikia mambo ya kiroho tu bila kushuka kwenye maisha halisi ya kila siku. Hivyo ni muhimu kutenda yote kwa nia ya kujenga, kuboresha maisha ya kikristo na kwa wokovu wa roho za watu. Jitihada zozote ziwe binafsi au za taasisi ambazo hazileti matunda hayo, inabidi zitazamwe upya kwani zitakuwa na mapungufu, amesisitiza Baba Mtakatifu Francisko.

Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.