2017-06-17 16:53:00

Mapambano dhidi ya umaskini, njaa, ugaidi na mabadiliko ya tabianchi


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 17 Juni 2017 amekutana na kuzungumza na  Chancellor Angela Merkel wa Ujerumani ambaye pia alibahatika kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paulo Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje  na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wameridhika na uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Ujerumani.

Baadaye, wameendelea kujikita katika masuala ya kitaifa na kimataifa kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa mkutano wa G20 utakaofanyika huko Humburg na kwamba, Ujerumani inapenda kukazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kikamilifu ili kupambana na baa la umaskini na njaa duniani; vitendo vya kigaidi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko ametoa salam zake za rambi rambi kufuatia kifo cha Chancellor mstaafu wa Ujerumani Helmut Kohl aliyefariki dunia, Ijumaa, tarehe 16 Juni 2017. Ni kiongozi aliyejisadaka kwa ajili ya umoja wa Ujerumani na umoja wa Jumuiya ya Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.