2017-06-16 15:46:00

Tambueni kuwa ninyi ni wadhaifu mnahitaji nguvu ya Mungu!


Viongozi wa Kanisa wanapaswa kutambua kwamba, dhamana na utume wao ni hazina ambayo imehifadhiwa katika vyombo vya udongo ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mwenyezi Mungu na wala si kutoka kwao. Katika maisha na utume wao, wanazongwa zongwa na shida pamoja na changamoto za maisha, hali inayowakumbusha kwamba, wao ni dhaifu, wanaweza kuelemewa na kubwagwa chini kutokana na udhaifu wao wa kibinadamu, lakini, neema ya Mungu ina uwezo wa kuwaganga, kuwaponya na kuwainua tena juu.

Hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake, bali kila mwamini anahitaji nguvu, baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo neema inayotiliwa mkazo na Mtakatifu Paulo, anapowaandikia Wakorintho kuhusu uwepo wa Kristo katika huduma ya Mtume! Haya ni mang’amuzi ambayo yanapaswa kuwasaidia waamini wote kutambua na kukiri kwamba wao ni wadhambi na kwamba, hazina yao kuu ni Kristo Yesu! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 16 Juni 2017 wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican.

Nguvu ya Mungu ina uwezo wa kuganga, kuponya na kumwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na udhaifu wake wa kibinadamu! Kwa kutambua udhaifu huu, waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kukimbilia na kuambata nguvu ya Mungu katika maisha yao. Tatizo kubwa katika maisha ya waamini ni pale wanaposhindwa kujitambua kwamba, wao ni wadhambi na kwamba, wanaelea katika dimbwi la udhaifu wa mwili. Mtakatifu Paulo anakaza kusema katika maisha wanakumbana na dhuluma, dhiki na nyanyaso; wanaona shaka, bali hawakati tamaa. Waamini wanapaswa kukubaliana na hali yao badala ya kuificha na kuanza kuishi kwa unafiki.

Waamini wawe na ujasiri wa kuondokana na tabia ya unafiki kwa kujichunguza kikamilifu, ili pale wanapogundua kwamba, ni wadhaiifu na wagonjwa wawe tayari kukimbilia na kuambata rehema na huruma ya Mungu katika maisha yao, vinginevyo, anasema Baba Mtakatifu Francisko ni waamini kuanza kutembea katika njia ya kiburi, majivuno, utupu wa maisha pamoja na kujitafuta wenyewe! Wale wasiojisikia kuwa wadhaifu wanatafuta utimilifu wa wokovu wao binafsi na kusahau kwamba, wanaokolewa tu kwa nguvu ya Mungu kama anavyokiri Mtakatifu Paulo.

Licha ya magumu na changamoto za maisha, Mtume Paulo hakati wala kukatishwa tamaa, kwani anatambua nguvu ya Mungu inayookoa. Kishawishi kikuu anachoweza kukabiliana nacho mwamini ni kushindwa kutambua udhaifu wake na kwamba dhamana na utume wake umehifadhiwa katika chombo cha udongo! Dhamana ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu iwajengee viongozi wa Kanisa bidii ya majadiliano kati ya hazina ambayo ni Kristo Yesu na udhaifu wao wa kibinadamu, ili kuwa watu wa kweli na waaminifu mbele ya Mungu. Dhambi itajwe na kuungamwa bila ukakasi wala aibu, ili kutoa nafasi kwa nguvu ya Mungu iweze kupenya. Waamini wakiweza kufikia hatua hii, watakuwa na furaha isiyokuwa na kipimo.

Siku ile ya Alhamisi kuu, Yesu alipokuwa anawaosha mitume miguu, alipofika kwa Mtakatifu Petro alikataa kuoshwa na Yesu, lakini alishindwa kutambua kwamba, kama binadamu anaelemewa na udhaifu wake, ni sawa na chombo cha udongo, kilichokuwa kinahitaji nguvu ya Mungu, ili kumwinua na kumwokoa kutoka katika dimbwi la aibu. Katika ukarimu wa kujitambua kuwa ni mdhambi na mdhaifu, mwamini anaweza kuanza safari ya kujikubali na kuambata: nguvu, huruma na upendo wa Mungu. Nguvu ya Mungu ni chemchemi ya utimilifu wa maisha ya kitume, wokovu na furaha ya kukombolewa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.