2017-06-15 13:44:00

Sakata la Makinikia Tanzania lapata sura mpya! Kimeeleweka!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Prof. John L. Thornton, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited na kukubaliana kuwa kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake nchini humo.

Prof. John L. Thornton ambaye amesafiri kwa ndege binafsi kutoka nchini Canada hadi Tanzania amekutana na Mhe. Rais Magufuli siku ya Jumatano, tarehe 14 Juni 2017, Ikulu Jijini Dar es Salaam. Mazungumzo yao yamehudhuriwa pia na Mhe. Ian Myles, Balozi wa Canada nchini Tanzania na Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Sheria na Katiba nchini Tanzania. Baada ya Mazungumzo hayo Prof. John L. Thornton amesema kwamba, kampuni yake ipo tayari kufanya mazungumzo na Tanzania, mazungumzo yatakayozingatia maslahi ya pande zote mbili na pia ipo tayari kulipa fedha zote ambazo inapaswa kulipa kwa Tanzania.

Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amesema, Serikali inakaribisha mazungumzo hayo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na kampuni ya Barrick Gold Corporation ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini Tanzania kwa maslahi ya pande zote mbili. Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kukubali kulipa fedha zinazodaiwa, Prof. John L. Thornton amekubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu (smelter) nchini humo.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amevionya vyombo vya habari vinavyowataja Marais wastaafu Mhe. Benjamin William Mkapa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete na kuwahusisha na taarifa za kamati mbili za uchunguzi wa madini yaliyo katika makontena yenye mchanga wa madini (Makinikia) ambapo ripoti zimekabidhiwa kwake na kamati hizo. Mhe. Magufuli amesema kwamba, amesoma taarifa za kamati zote mbili na hakuna mahali ambapo Marais wastaafu wametajwa, hivyo vyombo vya habari visiwachafue wazee hao, na viwaache wapumzike kwa utulivu baada ya kazi kubwa waliyofanya kulitumikia taifa.

Taarifa hizi zimetolewa na Ndugu Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais wa Tanzania, Jijini Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.