2017-06-15 16:00:00

Mabaraza ya Maaskofu Katoliki na Maaskofu kuongezewa madaraka!


Baraza la Makardinali Washauri lililoanza mkutano wake wa XX chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 12 Juni 2017, limehitimisha mkutano wake, Jumatano, tarehe 14 Juni 2017 kwa kukazia umuhimu wa kuimarisha huduma ya Vatican kwa ajili ya Makanisa mahalia. Makardinali wote wamehudhuria isipokuwa Kardinali Sean Patrick O’Malley aliyekuwa na dharura ya ugonjwa. Makardinali washauri wameonesha nia ya kuhamishia baadhi ya madaraka kutoka kwenye Mabaraza ya Kipapa mjini Vatican na kuyapeleka kwa Maaskofu Mahalia au kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili kuboresha huduma kwa familia ya Mungu kwenye Makanisa mahalia.

Kati ya masuala yanayopendekezwa kurudishwa kwenye Makanisa mahalia ni mchakato wa uteuzi wa Mapadre wanaofaa walau kuteuliwa kuwa Maaskofu mahalia kwa ajili ya kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Dhamana hii inaweza kupanuliwa na kuwahusisha watawa pamoja na viongozi wa waamini walei. Makardinali wameendelea kupembua Mabaraza mbali mbali ya Kipapa na kwa namna ya pekee, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.

Makardinali wamepitia na kujadili mapendekezo yatakayotolewa kwa Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuyafanyia maamuzi ni kuhusiana na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini; Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki pamoja na Mahakama kuu za Vatican: Mahakama Kuu ya Kanisa; Mahakama Kuu ya Rufaa ya Kipapa na Mahakama ya Toba ya Kitume. Makardinali wamehabarishwa pia mchakato wa mabadiliko yanayoendelea kutekelezwa katika Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican, kwa kuratibu rasilimali watu na vitu katika masuala ya kiuchumi pamoja na kuangalia mwenendo wa utekelezaji wa bajeti ya Vatican katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya Mwaka 2017.

Monsinyo Dario Eduardo Vigano’, amewasilisha mchakato wa mageuzi unaoendelea kutekelezwa na Sekretarieti ya mawasiliano mjini Vatican; kwa kuonesha mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika masuala ya kiuchumi na kiutawala. Baraza la Makardinali Washauri, litakutana tena katika mkutano wake wa XXI kuanzia tarehe 11- 13 Septemba 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.