2017-06-12 11:18:00

Waamini yaelekezeni mawazo yenu kwenye Fumbo la Utatu Mtakatifu


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 11 Juni 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mara baada ya tafakari ya Fumbo la Utatu Mtakatifu lililofunuliwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake kama Uso wa Mungu Mmoja katika Nafsi Tatu, zinazofumbatwa katika upendo unaowaunganisha wote katika: kazi ya uumbaji, ukombozi na kutakatifuza yaani: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, alimgeukia Mwenyeheri Itala Mela!

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 10 Juni 2017, huko Spezia, nchini Italia, alimtangaza Mtumishi wa Mungu Itala Mela kuwa Mwenyeheri! Itala Mela alizaliwa na kukulia katika familia iliyokuwa mbali sana na imani! Katika ujana wake akajitia “kiburi” na kujitangaza kuwa ni mkanimungu, lakini baadaye, akatubu na kumwongokea Mungu baada ya kupata mang’amuzi ya ndani kabisa ya maisha ya kiroho. Tangu wakati huo, akasimama na kujitoa bila ya kujibakiza; akazama katika huduma kwa vyuo vikuu vya Kikatoliki.

Katika safari ya maisha na wito wake, akabahatika kuwa ni Mtawa wa Shirika la Wabenediktini, akafanya tafakari ya kina kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu, ambalo Mama Kanisa ameliadhimisha Jumapili, tarehe 11 Juni 2017. Maisha na ushuhuda wa Mwenyeheri Itala Mela anasema Baba Mtakatifu Francisko unawatia shime waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuelekeza daima mawazo yao kwenye Fumbo la Utatu Mtakatifu yaani: Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu; Fumbo linalohifadhiwa katika sakafu ya mioyo wa waamini! Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwasalimia na kuwatakia heri na baraka mahujaji wote kutoka ndani na nje ya Italia, walioungana naye katika Sala ya Malaika wa Bwana, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.