2017-06-12 11:34:00

Kongamano la Kwanza la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Angola!


Kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha na utume wa Kanisa nchini Angola, Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, kuanzia tarehe 12 Juni 2017 linaadhimisha Kongamano la Kwanza la Ekaristi Takatifu Kitaifa na kilele cha maadhimisho haya ni tarehe 18 Juni 2017, Kanisa linapoadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Manuel Clemente, Patriaki wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kumwakilisha katika maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Angola, ili kuhamasisha imani kwa Kristo Yesu anayejisadaka kila siku katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kongamano hili linaadhimishwa katika Jimbo kuu la Huambo.

Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia Kardinali Clemente anakaza kusema Liturujia ni kilele ambamo kazi ya Kanisa inaelekea, na papo hapo ni chemchemi zinamotoka nguvu zake zote. Maana bidii zote za kazi za kitume hukusudiwa ili wote, waliofanywa watoto wa Mungu kwa njia ya imani na ubatizo, wakusanyike pamoja, wamtukuze Mungu katika Kanisa, washiriki sadaka na kuila karamu ya Bwana. Hii ni changamoto kwa waamini kuishi “umoja wa utakatifu na ushuhuda wa imani”; wawe tayari kuundwa upya kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, linalowawashia moto wa upendo wenye bidii kutoka kwa Kristo Yesu! Kwa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwenyezi Mungu hupewa sifa na utukufu katika Kristo Yesu na mwanadamu hutakaswa kwa neema na baraka zinazomiminika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. 

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume “Sacramentum Caritatis” yaani  “Sakramenti ya Upendo”  anasema, Ekaristi Takatifu ni fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa; ni kiini na moyo wa Kanisa. Ni Fumbo la upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Utatu Mtakatifu, kwani Yesu mwenyewe anajitoa kuwa sadaka na chakula cha uzima wa milele. Ekaristi Takatifu inafunua mpango wa upendo wa Mungu ambao unaongoza historia nzima ya ukombozi.

Ekaristi Takatifu inawashirikisha waamini uhai wa Mungu mwenyewe. Kumbe, Ekaristi Takatifu ni Fumbo la imani inayofumbatwa katika upendo wa Utatu Mtakatifu, Fumbo ambalo waamini wanaitwa kwa neema kulishiriki kikamilifu kwa kushangaa pamoja na Mtakatifu Agustino anayesema, kama utaona upendo, utaona Utatu Mtakatifu!  Papa Francisko katika barua yake kwa Kardinali Manuel Clemente, Patriaki wa Jimbo kuu la Lisbon anayemwakilisha katika maadhimisho ya Kongamano la Kwanza la Ekaristi Takatifu nchini Angola anasema, Ekaristi Takatifu ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, kwamba mtu akile na wala asife. Yesu mwenyewe anakaza kusema kwamba, Yeye ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, mtu akila chakula hiki ataishi milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.