2017-06-10 15:46:00

Vatican kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Italia!


Matumaini yanayofumbatwa katika kumbu kumbu endelevu ya wazee waliojisaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Italia; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; kwa kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa! Changamoto mamboleo ziwe ni fursa ya kukuwa na kukomaa zaidi la wala zisiwe ni sababu za kuwakatisha watu tamaa! Changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira, tunu msingi za kifamilia; maisha na utume wa Kanisa nchini Italia ni mambo yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa!

Haya ni kati ya mambo mazito yaliyozungumzwa na Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Ikulu ya Italia na kuzungumza na Rais Sergio Mattarella wa Italia, Jumamosi, tarehe 10 Juni 2017. Baba Mtakatifu amemshukuru Rais Mattarella kwa kumtembelea mjini Vatican tarehe 18 Aprili 2015, muda mfupi tu, baada ya kuchaguliwa kuiongoza familia ya Mungu nchini Italia kama Rais. Mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee hata katika Katiba ya Italia ni: utu wa binadamu, familia na kazi, chemchemi ya matumaini kwa familia ya Mungu nchini Italia.

Italia inapaswa kuendelea kushirikiana kikamilifu na Jumuiya ya Kimataifa ili kukabili changamoto mamboleo kama vile: vitendo vya kigaidi, misimamo mikali ya kidini; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linalotokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kiuchumi sehemu mbali mbali za dunia, hali inayogumisha pia maisha ya ndoa na familia.

Baba Mtakatifu anaishukuru na kuipongeza familia ya Mungu nchini Italia na kuitaka sasa kutumia amana na utajiri wake wa maisha ya kiroho na kiutu ili kugeuza changamoto zote hizi kuwa ni fursa ya kukua na kukomaa. Anaipongeza Italia kwa huduma makini ya kuokoa na kuwatunza wakimbizi na wahamiaji; katika kulinda na kudumisha: ulinzi na usalama sehemu mbali mbali za dunia sanjari na ushirikiano wa kimataifa. Baba Mtakatifu amewapongeza wananchi wote wa Italia ya kati walioguswa na kutikiswa kwa tetemeko la ardhi, lakini kutokana na imani yao thabiti, ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa wameweza kusimama tena! Matokeo yote haya ni ushuhuda unaobubujika kutoka katika imani kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukosefu wa fursa za ajira ni changamoto pevu kwa familia ya Mungu nchini Italia! Kuna maelfu ya watu wasiokuwa na kazi, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; kuna umaskini wa hali na mali; vijana wanashindwa kufanya maamuzi magumu katika maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anasema, rasilimali fedha inapaswa kuwekezwa katika sera na mipango ya muda mrefu ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi. Kazi isaidie pia kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kukuza mahusiano mema ndani ya jamii. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Italia ili kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli kwa njia ya mafungamano ya kijamii! Hakuna mtu anayeweza kujidai kwamba, anaweza kutatua kero na changamoto za Italia peke yake!

Baba Mtakatifu analitaka Kanisa nchini Italia kuwa kweli ni sauti ya kinabii, kwa kuandamana na familia ya Mungu wakati wa raha, shida na matumaini. Kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi mintarafu Mkataba wa Laterano uliofanyiwa marekebisho kunako mwaka 1984. Italia imebahatika kuwa na Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Duniani. Mkataba wa Mwaka 1929 unaweka  bayana dhamana na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hali ambayo imeboreshwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano mwema kati ya Serikali ya Italia na Vatican. Matunda ya ushirikiano mwema katika siku za hivi karibuni ni maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambao umeadhimishwa kwa amani na utulivu na hivyo kuwawezesha waamini kupata matunda ya kiroho yaliyokusudiwa. Vatican inaishukuru sana, Serikali ya Italia na kwamba, pande hizi mbili zitaendelea kushirikiana na kushikamana ili kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zinazojitokeza katika safari yao kwa ajili ya mafao ya wengi. Kanisa, Vatican na Serikali ya Italia vitaendelea kuwajibika na kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo makini ya watu wa Mungu nchini Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.