2017-06-09 14:18:00

Nguvu ya ziada kuokoa meli inayozama kwenye umaskini wa kupindukia


Lazima kuongeza nguvu ili kuwaopoa watu wanaozama kwenye umaskini wa kutupwa. Katika hotuba yake, Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, Uswiss, katika kikao cha 35 cha Baraza la Usalama na Haki za Binadamu, anasema kwamba kwa sasa asilimia moja tu (1%) ya wanadamu duniani, ndio wanaomiliki asilimia tisini na tisa (99%) ya mali iliyopo duniani, na kupelekea ukosefu mkubwa wa uwiano kati ya matajiri na maskini.

Umaskini unaokithiri katika jamii leo, sio takwimu za kwenye makaratasi au kwenye mitandao, bali ni uhalisia wa maisha ambao ni lazima kuushughulikia kama changamoto kwa kuwashirikisha binadamu wote, hasa wanyonge, na kuleta usawa kwa kila binadamu kijamii na kiuchumi. Katika hilo, izingatiwe sana heshima kwa utu wa binadamu.

Askofu mkuu Ivan Jurkovic anasisitiza kumfanya kila mmoja awe mshiriki hai katika kuboresha maisha yake, huku kanuni za mshikamano na mgawanyo wa wajibu zikizingatiwa. Wanadamu wote wapewe fursa ya kufikia rasilimali za maendeleo ili kufikia ile hali ya maisha inayoruhusu kuishi kwa utulivu na furaha. Haya yanawezekana iwapo kila mmoja atawajibika kukabili changamoto za maisha, kutetea haki hasa za wanyonge na kuheshimu utu wa kila binadamu, kwani kaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kila mpango na kila shughuli ilenge kunufaisha jamii nzima kwa manufaa ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake ya Kitume, Evangelii Gaudium, yaani Furaha ya Injili, anafundisha kwamba ukuaji wa uwiano kati ya watu ni jambo linalokwenda mbali zaidi ya uchumi peke yake, ni jambo linalohitaji uamuzi, mikakati, mfumo na taratibu zinazolenga ugawaji sawa wa rasilimali, mapato, nafasi za kazi na ushirikishaji wa maskini na wanyonge katika shughuli za maendeleo. Lazima kupiga vita ubinafsi na kujenga utamaduni wa ukarimu.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.