2017-06-08 14:05:00

Wanavyuo Roma waalikwa kujifunza kupenda na sio kutafuta kupendwa


Lorenzo Leuzzi, Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Roma, anawaandikia wanafunzi wa vyuo vikuu Roma, akiwaalika wajifunze kupenda na sio kutafuta kupendwa. Katika barua yake hiyo anatoa mfano wa Mt. Justin, aliyekufa shahidi wakati Dola ya kirumi inamshutumu kuwa ni Mkani-Mungu. Ni jambo la kuchekesha mkristo kushutumiwa kuwa ni Mkani-Mungu, hata hivyo Askofu Lorenzo Leuzzi anasema, ni jambo la kufikirisha zaidi kwamba jamii hiyo ya kirumi kwa miaka ya 163 wakati wa utawala wa Marc Aurelio, ilikuwa ni jamii iliyonuia kuwa jamii ya Ukani-Mungu, lakini leo hii ni jamii ya kidini sana, na ni ya kidini hakuna mfano.

Kuwa mcha Mungu au jamii ya kidini maana yake ni kuwa tegemezi, kama vile watu walivyo tegemezi leo kwenye mitandao ya kijamii. Mwanadamu leo anapenda kuwa tegemezi sababu hapendi magumu, hapendi matatizo. Suluhu anaiona kwenye kumtegemea mtu mwingine ili awe na uhakika wa kila anachohitaji. Hata hivyo mitandao jamii haiwezi kukuhakikishia kila kitu, wakati kuwa mcha Mungu, kuwa mtu wa dini, una uhakika wa usalama wa maisha ya kila siku na utulivu wa maisha baada ya kifo. Mt. Justin alifundisha kuwa Mungu katika Kristo Yesu, hakuwa na nia ya kutafuta kupendwa, bali anaonesha namna ya kupenda kweli kwa dhati.

Jamii ya leo inatengeneza watu tegemezi wanaotafuta kufanyiwa kila kitu, wanaotafuta kupendwa. Utegemezi huu haufai, anasema Askofu Leuzzi, badala yake inafaa kujifunza kupenda na kujali wengine, wakati huo huo mtu akijiweka katika kumtegemea Mungu kwa yale ambayo yanazidi uwezo wake. Hii ni changamoto kwa jamii ya leo, kutafuta kupendwa hata kufikia hatua ya kuwa mkatili, au kulazimisha wengine wakupende. Ni wakati wa kujibu kwa ufasaha swali ambalo Kristo anamuuliza Petro: Petro wa Simone, je unanipenda? Ukijibu swali hilo kwa ufasaha, litabadili maisha yako, sababu Mungu anakualika kupenda kwa uaminifu na kwa moyo wote, na sio kutafuta kupendwa.  

Askofu Leuzzi, anawaalika wanafunzi wa vyuo vikuu kutokuwa na hofu ya kubadili jamii, wawe mashuhuda kweli wa kupenda na sio kutafuta kupendwa. Katika kipindi cha likizo kubwa, Jimbo kuu la Roma, kupitia mapadri walezi wa wanafunzi wa vyuo, linaandaa hija mbali mbali kwenda madhabahu za Bikira Maria wa Fatima na Lourdes. Wenye nia ya kushiriki wanaalikwa kuwasiliana na mapadri walezi.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.