2017-06-08 15:43:00

Sikilizeni na kujibu kilio cha mahangaiko ya watu wenye njaa duniani!


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada, CCCB, kwa kuguswa na mahangaiko ya watu wa Sudan ya Kusini, Yemen, Nigeria na Somalia linaungana na viongozi wa dini mbali mbali nchini Canada ili kushikamana kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanaotoka katika nchi hizi ambazo kwa sasa zinakabiliwana hatari kubwa ya baa la njaa na umaskini wa kutupwa kutokana na ukame wa muda mrefu, vita pamoja na mipasuko ya kijamii.  Kunako mwezi Februari 2017 Umoja wa Mataifa ulitangaza kwamba, kuna watu milioni 20 kati yao kuna watoto milioni 1. 4 wanaokabiliwa na hatari ya kufa kwa njaa katika kipindi cha muda mfupi kuanzia sasa!

Umoja wa Mataifa haujafanikiwa kukusanya fedha inayohitajika kwa ajili ya kugharimia mchakato wa upatikanaji wa chakula cha katika maeneo yaliyoathirika kwa ukame wa kutisha, vita na mipasuko ya kijamii. Viongozi wa kidini wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwakumbuka katika sala na dua zao wananchi wa Sudan ya Kusini, Yemen, Nigeria na Somalia. Waendelee kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu kwani pasi na amani, hakuna ustawi, maendeleo wala mafao ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema, Shirika la Kanisa Katoliki la Maendeleo na Amani nchini Canada, kwa sasa linajipanga kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa kukusanya fedha kwa ajili ya kusaidia kugharimia upatikanaji wa chakula. Kuanzia tarehe 17 Machi hadi 30 Juni 2017, Shirika hili la misaada kwa kushirikiana na Serikali ya Canada linatakusanya fedha kwa ajili ya kusaidia nchi zilizoathirika kwa ukame, vita na mipasuko ya kijamii. Maaskofu wanaiomba familia ya Mungu nchini Canada kujadiliana ili kuweza kuwa kweli ni sauti ya kinabii kwa ajili ya mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia.

Viongozi wa kidini nchini Canada wanasikitika kusema,  vita na machafuko ya kijamii na kikabila ni chanzo kikuu cha baa la njaa nchini Sudan ya Kusini, Yemen, Nigeria na Somalia. Umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimamia sheria, kanuni na taratibu za kimataifa, ili kweli haki, amani na utulivu viweze kurejeshwa tena katika nchi hizi ambazo watu wasiokuwa na hatia wanaendelea kuteseka sana! Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linasema, licha ya kusali na kuzungumza, lakini watu waguswe sana na mahangaiko ya wananchi hawa ili kuwasaidia kwa kuchangia kwa hali na mali!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.