2017-06-08 12:12:00

Msamaha na upatanisho wa kweli uvunje kuta za utengano kati ya watu!


Kardinali Luis Antonio G. Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2017 amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia walimwengu zawadi ya amani, ambayo kimsingi ni chachu ya maendeleo, msamaha, upatanisho na maridhiano kati ya watu wa mataifa! Dunia imejawa na hofu ya vita na mashambulizi ya kigaidi kutoka sehemu mbali mbali za dunia!

Hivi karibuni, kumekuwepo pia na shambulizi la kigaidi huko nchini Ufilippini. Kwa sasa kuna mapambano kati ya Serikali na vikundi vya kigaidi ambavyo tangu mwezi Mei, 2016 vimemekuwa vikifanya mashambulizi ya kushtukiza na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Mashambulizi haya yanaendelea kusababisha wananchi kukosa imani na serikali yao mintarafu ulinzi na usalama; yanabomoa mafungamano ya kijamii pamoja na kusababisha watu kuwa na maamuzi mbele kwa mambo ya kidini.

Waamini wanapaswa kumwomba Roho Mtakatifu awakirimie paji na umoja, upendo na mshikamano badala ya hali ya sasa inayoendelea kupandikiza mbegu ya kifo, chuki na uhasama kati ya watu! Wamwombe Roho Mtakatifu asaidie kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, badala ya ujenzi wa kuta zinazotokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; ambayo pengine ina malengo ya muda mfupi kwa mfano kuweza kushinda uchaguzi mkuu au kuganga njaa, lakini madhara yake kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni makubwa sana! Hali inatisha sana kwa matajiri wanaendelea kutajirika zaidi wakati maskini wanaendelea kuzama na kutopea katika umaskini wa hali na kipato! Lakini, takwimu zinaonesha kwamba, ikiwa kama utajiri na rasilimali ya dunia itaweza kutumiwa vyema, inaweza kusaidia kupambana na baa la umaskini duniani! Uchoyo na ubinafsi utaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika majanga ya maisha! Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, watambue umuhimu wa kushirikishana karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Karama za Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mshikamano kati ya watu, ni zawadi kwa ajili ya huduma makini kwa familia ya Mungu! Mapaji ya Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya wengi na wala si kwa ajili ya mafao ya mtu binafsi peke yake! Umefika wakati kwa watu kuvunjilia mbali kuta za utengano kwa kuwajali na kuwathamini watu; kwa kusimamia misingi ya haki, amani na maridhiano. Watu wajenge utamaduni wa kuthamini utu na heshima ya binadamu; kwa kujikita katika toba msamaha na upatanisho wa kweli. Kusamahe ni mchakato wa kujiweka huru kutokana na chuki na hali ya kutaka kulipiza kisasi. Ikiwa kama waamini na watu wote wenye mapenzi mema wataweza kumwilisha  vyema karama za Roho Mtakatifu katika maisha yao, ulimwengu unaweza kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.