2017-06-07 09:10:00

Yote ni kwa ajili ya umoja na huduma katika Roho Mtakatifu


Katika mapambazuko ya millennia ya tatu ya Ukristo, waamini wanahamasishwa zaidi na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha! Ni kipindi cha kujikita katika majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika maisha ya sala, kwa kushirikiana na waamini wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo ili kuweza kuombea umoja wa Kanisa. Ni muda wa kushikamana katika huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa.

Ni ushuhuda unaopaswa kusimikwa katika maisha ya kiroho, kwa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo katika vipaumbele vya maisha. Uekumene wa damu ni changamoto endelevu kwa waamini sehemu mbali mbali za dunia kutokana na wimbi la nyanyaso na dhuluma wanazofanyiwa Wakristo wote pasi na ubaguzi wa Makanisa wala Madhehebu yao! Haya ni mambo msingi yaliytojitokeza hata wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Wakarismatiki Wakatoliki Duniani, tukio ambalo katika mkesha wa Sherehe ya Pentekoste kwa Mwaka 2017 limekuwasanya Wakristo kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbali mbali duniani, kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Padre Augustine John Temu kutoka Jimbo Katoliki la Tanga, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anaendelea kufafanua kuhusu umoja miongoni mwa Wakristo kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii.

Hii inatokana na ukweli kwamba, imani yao inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo na kwamba, wanaamini katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, Kristo Yesu ni Bwana na Mkombozi wa dunia. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake ameweza kuwakomboa wanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Wakarismatiki Wakatoliki Dunia imekuwa ni fursa ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene katika sala na maisha ya kiroho.

Kimekuwa ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani kwa mapungufu yaliyojitokeza katika kipindi chote hiki. Imekuwa ni fursa ya kumwimbia Roho Mtakatifu utenziwa shukrani kwa neema na baraka zake kwa Kanisa la Kristo, kwani Chama hiki kimetoa fursa kwa waamini kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao kwa njia matendo ya huruma. Maaskofu, Mapadre na viongozi mbali mbali wa Kanisa wanakumbushwa kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kuwalea, kuwaongoza na kuwasaidia Wakarismatiki kuweza kujitambua, kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuzingatia: sheria, kanuni na taratibu zinazotolewa na Mama Kanisa kwa waja wake .

Ni changamoto kubwa kwa waamini wengine kufungua akili na nyoyo zao ili kujifunza historia, maisha, utume na changamoto zinazowakabilia Wakarismatiki katika maeneo yao, tayari kuzivalia njuga kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo! Itasikitisha sana kuona “mbereko na mtoto vinatupwa kwa pamoja”. Ni muda anasema Padre Padre Augustine John Temu wa kuacha dharau kwa wengine na kutojiona kuwa ni bora zaidi kuliko wa waamini wengine wote kutokana na karama au mapaji waliyojaliwa na Roho Mtakatifu. Yote hii ni huduma katika Roho Mtakatifu, kwa ajili ya umoja, ustawi na maendeleo ya Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.