2017-06-07 15:16:00

Sala ya Baba Yetu ni chemchemi ya matumaini ya Kikristo!


Yesu aliwafundisha wanafunzi wake ile Sala kuu ya Baba yetu wa mbinguni, ambayo kimsingi ni chemchemi ya matumaini ya Kikristo. Mwinjili Luka ndiye anayefafanua kwa kina na mapana utume wa maisha ya Yesu katika Sala. Mitume walikuwa wanashangazwa na maisha ya Yesu ambaye daima kila siku asubuhi na jioni alijitenga na shughuli nyingine zote, akatumia muda wake kwa ajili ya sala! Wanafunzi baada ya kuona umuhimu wa sala katika maisha na utume wao, wakamwomba Yesu ili aweze kuwafundisha. Sala ya Baba Yetu ni Sala ya Kikristo inayowawezesha waamini kumwita Mwenyezi Mungu, “Baba Yetu”.

Sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni imefafanuliwa kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 7 Juni 2017 kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi kuhusu Matumaini ya Kikristo! Huu ni muhtasari wa Fumbo la Sala ya Kikristo, kwa kuwapatia waamini ujasiri wa kuthubutu kumwita Mwenyezi Mungu, “Baba Yetu”. Ni Sala inayoonesha uhusiano unaomwezesha mwamini kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, kama ambavyo mtoto anavyoweza kuthubutu kumwita, Baba yake, kwa kutambua kwamba anapendwa na kutunzwa naye. Haya ni mabadiliko makubwa ambayo yanaletwa na Ukristo katika saikolojia ya dini katika maisha ya mwanadamu!

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu anapenda kuwashangaza waja wake, kwa kuwafanya kujisikia wadogo kama “kidonge cha pilton”, bila kuwaogofya; kuwaponda wala kuwatesa. Haya ni mageuzi makubwa ambayo si rahisi sana kuweza kuyapokea katika moyo wa binadamu. Ikiwa kama wale wanawake walioshangazwa na Uufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kwa kuona kaburi tupu, kiasi hata cha kushangaa na kuogopa! Lakini, Yesu anawafunulia wafusi wake kwamba, Mwenyezi “Mungu ni Baba”.

Mfano wa Baba mwenye huruma unaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anawapenda watoto wake; anawahurumia na kuwajali, kiasi cha kuwagawia sehemu ya urithi wao. Ana thamini uhuru wa watoto wake na kwamba, Baba mwenye huruma aliyefunuliwa na Kristo Yesu. Ni Baba mwema anayewalinda na kuwapenda watoto wake. Hata pale Mwana mpotevu anaporejea kutoka mafichoni alikokwenda “kutumbua sehemu ya urithi wake na makahaba”, anathubutu tena kurejea nyumbani na kupokelewa kwa heshima na sherehe nzito ya kukata na shoka!

Hapa hakuna haki ya kibinadamu inayotumiwa bali anajikita zaidi katika msamaha na kwamba, kipindi chote kile alichokuwa ametoweka nyumbani kilimpatia majonzi makubwa sana moyoni mwake, alikosa upendo kutoka kwa Baba yake. Upendo wa Mungu ni kiini cha Fumbo la uwepo, maisha na utume wa Kanisa, kiasi hata cha waamini kuthubutu kumwita Mwenyezi Mungu “Abba”, neno ambayo Mtume Paulo katika Nyaraka zake  ameamua kuliacha kama lilivyo bila kulitafsiri kuwa “baba” Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, hawako pweke, hata kama wakiwa mbali kiasi gani; wakakosana na kupekenya kwa namna mbali mbali, lakini Yesu anawaambia wafuasi wake kwamba. Mwenyezi Mungu daima anawataka kuwa karibu na watu wake na kamwe hawezi “kucheza” mbali na watoto wake. Huu ndio uhakika wa chimbuko la matumaini ya Kikristo yanayofumbatwa katika taafsiri mbali mbali ya “Baba Yetu” uliye mbinguni. Waamini wanapokuwa na shida na mahangaiko mbali mbali wanaalikwa kumkimbilia Mwenyezi Mungu kwa imani na matumaini ili kuomba msaada!

Mwenyezi Mungu anaweza kuzima kiu ya mahitaji ya binadamu mintarafu: Chakula, afya, fursa za ajira pamoja na kuomba msamaha wa dhambi zinazobubujika kutokana na vishawishi na yale ambayo si rahisi sana kuyangalia katika maisha ya watu. Mwenyezi Mungu ni Baba wa wote anayewaangalia waja wake kwa jicho la upendo na kamwe hawezi kuwaacha bure wateseke! Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuzama katika Sala ya Yesu, ili kujenga uhusiano wa upendo na imani kwa Mwenyezi Mungu; uhusiano ambao unaondoa woga na wasi wasi katika maisha. Roho Mtakatifu anawawezesha watu wote kuwa ni watoto wapendwa wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.