2017-06-07 15:51:00

Nishati endelevu kwa matumizi endelevu ya binadamu!


Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu kuanzia tarehe 8 -11 Juni 2017 atakuwa mjini Astana, Kazakistan kuhudhuria Onesho la EXPO 2017 linaloongozwa na kauli mbiu “Nishati ya baadaye”. Kardinali Turkson anashiriki kama Kamishina wa Onesho hili ambalo linazishirikisha nchi nyingi, ikiwemo pia Vatican. Itakubukwa kwamba, Vatican imekuwa ikishiriki maonesho kama haya tangu mwaka 1815 kwa kuwa na banda lake binafsi ambalo kwa mwaka 2017 linaongozwa na kauli mbiu “ Nishati kwa mafao ya wengi: utunzaji wa nyumba ya wote”.

Kauli mbiu hii inafumbata matarajio ya Jumuiya ya Kimataifa mintarafu nishati rafiki, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Jukwaa hili limekamilika kwa ushiriki wa Kanisa mahalia! Lengo ni kutoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu pamoja na kujitahidi kuboresha mazingira nyumba ya wote, kwa kuwa na matumizi sawa na endelevu ya rasilimali asilia.

Banda la Vatican limetengenezwa kwa mfumo wa kidigitali kwa kuwashirikisha wasanii, wanazuoni na wataalam wa maisha ya kiroho wanaojadili kwa kina na mapana kuhusu: Upendo wa Mungu kama chanzo cha kazi ya uumbaji; nishati kama nyenzo msingi iliyowekwa mikononi mwa binadamu, nyenzo ambayo haijatumika barabara kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi; nishati inapaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mwishoni ni nguvu ya maisha ya kiroho inayooneshwa kwa nguvu ya sala; maana ya maisha na majadiliano ya kidini. Uzinduzi wa Onesho hili ni hapo tarehe 9 Juni 2017. Kardinali Turkson katika ziara hii ya kikazi anaongozana na Askofu mkuu Francis Assisi Chullikatt, Balozi wa Vatican nchini Kazakistan, Kirghizistan na Tagikistan pamoja na viongozi wa Kanisa mahalia. Siku ya Taifa la Vatican itakuwa ni tarehe 2 Septemba 2017.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.