2017-06-06 14:33:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 91 ya Kimissionari Duniani 2017


Utume ni kiini cha imani ya Kikristo ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 91 ya Kimissionari Duniani, inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 22 Oktoba 2017, yaani Jumapili ya mwisho ya Mwezi Oktoba. Katika ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa, anakazia umuhimu wa utume na nguvu ya mabadiliko iletwayo na Injili ya Kristo aliye njia, ukweli na uzima. Utume wa Kanisa uwawezeshe waamini kutembea pamoja na Kristo Yesu na kwamba, hii ni changamoto endelevu inayojikita katika mchakato wa hija ya Mama Kanisa. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, wao ni matumaini ya utume wa Kanisa na kwamba, Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari  yanapaswa kusaidia mchakato wa uinjilishaji hadi miisho ya dunia. Dhamana hii itekelezwe kwa kumshirikisha Bikira Maria, Mama wa Uinjilishaji!

Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu ndiye mwinjilishaji mahiri, anayeendelea kuita na kuwatuma waamini kwenda kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo wa Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kutafakari kwa kina na mapana kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kimissionari Duniani kwa kutambua kwamba, utume ni kiini cha imani ya Kikristo. Kwa asili Kanisa la Yesu ni la kimissionari, vinginevyo lingekwisha kutoweka katika uso wa dunia, changamoto kwa waamini ni kuendelea kutafakari kuhusu utambulisho, dhamana na wajibu wao kama waamini katika ulimwengu ambamo umegubikwa kwa vita inayowaathiri zaidi watu wasiokuwa na hatia. Waamini watambua msingi, kiini na mambo msingi wanayopaswa kuyatekeleza katika maisha yao.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utume wa Kanisa unaelekezwa kwa watu wote wenye mapenzi mema na unasimikwa katika msingi wa Injili inayoleta mabadiliko; inayoshirikisha furaha kwani ni chemchemi ya maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka, alieyawapelekea mitume wake Roho Mtakatifu na hivyo inakuwa ni: Njia, Ukweli na Uzima. Ni njia kwani waamini wanaalikwa kumfuasa Kristo Yesu kwa imani na ujasiri; kama Njia ili kuonja Ukweli na kupokea Uzima kiini cha umoja na Baba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, anayewawezesha kuwa huru kutoka kwenye mifumo yote ya ubinafsi kwani yeye ni chemchemi ya ubunifu katika upendo.

Mwenyezi Mungu anawataka waja wake kuleta mageuzi makubwa kwa watoto wake wanaoweza kumwabudu katika roho na ukweli, katika maisha yanayorutubishwa na Roho Mtakatifu kwa kumwiga Kristo Yesu kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu Baba, kwani utukufu wa Mungu unajionesha kwa binadamu aliye hai. Kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema, Injili inakuwa ni Neno la uzima na lenye nguvu linapotangazwa, yaani Yesu Kristo anayeendelea kujitwalia mwili katika hali mbali mbali za maisha ya binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, utume wa Kanisa si kwa ajili ya kusambaza wazo kuhusu dini au kanuni maadili bali kwa njia ya Kanisa ni kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu anaendelea kuinjilisha na kutenda, huku akitembea pamoja na waja wake, muda muafaka wa wokovu katika historia. Kwa kutangaza na kushuhudia Injili, Kristo Yesu anakuwa ni mwenza katika safari na kwa mwamini anayempokea kwa imani na mapendo anapata nguvu ya Roho wake anayeboresha maisha ya waja wake kama inavyotenda mvua kwa viumbe vyote vya Mungu. Ufufuko wa Kristo siyo tukio la kale, unayo nguvu muhimu ambayo imeupenya ulimwengu huu. Pale ambapo kila kitu kinaonekana kana kwamba, kimekufa, hapo wema huweza kuchipua katika ufufuko! Hii ndiyo nguvu ya ufufuko isiyokuwa na mfano!

Baba Mtakatifu anasema, chanzo cha Ukristo ni pale ambapo mtu anakutana na Yesu na kuyapatia maisha mwelekeo mpya! Kumbe, Injili ni Kristo Mwenyewe anayeendelea kujisadaka na kuita ili watu waweze kumpokea kwa imani na unyenyekevu mkuu, ili kushiriki kikamilifu katika maisha ya Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Injili inakuwa ni chanzo cha maisha mapya, huru na maondoleo ya dhambi; ni maisha angavu yaliyogeuzwa kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara, maisha yanaimarishwa kwa njia ya Roho Mtakatifu anayewawezesha waamini kutembea katika njia mpya na kuwa ni mashuhuda. Kwa njia ya Ekaristi, Yesu anakuwa ni chakula cha watu wapya na dawa ya maisha ya uzima wa milele.

Ulimwengu unahitaji Injili ya Kristo ambaye kwa njia ya Kanisa lake anaendeleza utume wa kuwa ni Msamaria mwema, anayeganga na kuponya madonda ya mwanadamu yanayoendelea kuvuja damu; anakuwa ni Mchungaji mwema, anayejitaabisha kuwatafuta Kondoo waliopotea. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote wanaoendelea kujitaabisha kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na vita, chuki na mipasuko ya kijamii. Katika mazingira haya magumu na hatarishi, Yesu bado anaendelea kuwa ni faraja na nguvu ya watu wake. Ushuhuda wa Injili unawasaidia waamini kuvuka tabia ya kujifungia katika ubinafsi wao, vita, kinzani, ubaguzi na ukabila kwa kuanza kujielekeza katika upatanisho wa wote, udugu na ushirikiano.

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kukumbusha kwamba, utume wa Kanisa unafumbatwa katika tasaufi kutoka katika ufahari wake na kwenda pembezoni mwa maisha na vipaumbele vya watu ili kuwawashia mwanga wa Injili. Hii ni changamoto ya hija ambayo kimsingi ni endelevu na inayopita katika majangwa ya maisha ya watu wenye njaa na kiu ya ukweli na haki. Ni utume unaomwezesha binadamu kutambua kwamba daima yuko uhamishoni na kwamba, hapa duniani anayo makazi ya muda tu; daima anatamani kwenda mbinguni. Utume wa Kanisa ni daraja kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, unaotekelezwa na Kanisa, Fumbo la mwili wake mtukufu.  Ni heri kuwa na Kanisa lililochubuka, lenye maumivu na lililochafuka, badala ya Kanisa gonjwa, lililojifungia katika ubinafsi wake kwa kung’angania usalama wake tu.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kwamba, wao ni matumaini ya utume wa Kanisa, Yesu na Habari Njema, inayoendelea kuwavuta vijana wengi duniani, kumbe wanapaswa kuwa na ujasiri, utakaowasaidia kujitosa kimasomaso kwa ajili ya huduma kwa binadamu kama watu wa kujitolea; vijana wanaojisadaka kwa ajili ya ushuhuda wa Kristo na Kanisa lake. Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakatoadhimishwa kunako mwezi Oktoba, 2018 inaongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito” fursa makini ya kuwashirikisha vijana katika uwajibikaji wa kimissionari unaohitaji uwepo wa vijana wenye mang’amuzi na kipaji cha ubinifu.

Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwamba, Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari ni chombo madhubuti kinachowahamasisha Wakristo kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wote; katika uhalisia wa maisha ya kila siku; kwa njia ya malezi na majiundo makini ya familia ya Mungu, ili kweli ari na moyo wa kimissionari uweze kuwaambata wote. Siku ya Kimissionari Duniani ni muda muafaka na kiini cha umissionari wa Jumuiya ya waamini inayoshiriki katika sala, ushuhuda wa maisha na umoja katika rasilimali vitu, ili kujibu changamoto ya uinjilishaji.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa Bikira Maria, Mama wa Uinjilishaji ambaye kwa njia ya Roho Mtakatifu alimpokea Neno wa Mungu na kuzama katika undani wa imani yake. Awasaidie waamini kukubali mwaliko huu juu ya dharura ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Yesu. Awaombee ili waweze kuwa na ari na nguvu mpya kuwatangazia wote Injili ya uhai inayoshinda kifo. Awaombee ili waweze kuwa ni watakatifu kwa kutafuta njia mpya, ili zawadi ya wokovu wa Mungu iweze kuafikia watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.