2017-06-06 13:14:00

Baraza la Maaskofu Zimbabwe, Katiba izingatiwe kwenye uchaguzi wa 2018


Kwa kuzingatia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani 2018, maaskofu wa Zimbabwe, Jumapili ya Pentekoste, tarehe 4 Juni 2017, wametoa barua ya kichungaji kuhusu, Uchaguzi, Amani na Maendeleo, wakiwaalika waamini kukataa kila aina ya machafuko, uonevu na ukandamizaji wa kulazimishwa kufanya mambo kinyume cha dhamiri zao, kwani ni mambo yanayopelekea kuvuruga uchaguzi wa haki, na hivyo kutokuwa na imani juu ya uhalali wa uchaguzi.

Maaskofu Zimbabwe wanasisitiza kwamba serikali ya Rais Robert Mugabe ni lazima ihakikishe raia wanafurahia na kufaidika na haki zao za kiraia na uhuru wao wa kujieleza, kiasi cha kuweza kufanya maamuzi kwa uhuru wakiongozwa na dhamiri zao safi. Katika barua hiyo ya kichungaji, Baraza la Maaskofu Zimbabwe, wanaalika vyama vyote vya kisiasa, serikali iliyo madarakani, na kila raia wa Zimbwabwe waheshimu na kufuata kwa uaminifu Katiba ya nchi yao iliyopitishwa kwa shauku kubwa katika kura za maoni kunako mwaka 2013. Kwa namna hii watahakikisha kuwapo kwa amani, heshima kwa utu wa binadamu, na kudhihirisha upendo na utii kwa Mungu, aliye Baba wa wanadamu wote.

Ikumbukwe kwamba baada ya taabu za kisiasa na uchaguzi mnamo 2008 zilizopelekea machafuko nchini Zimbabwe, na myumbo mkubwa wa uchumi nchini humo, ililazimika kutia mkwaju wa makubaliano ya uongozi wa serikali ya mseto kati ya chama cha ZANU-PF na vyama viwili vya kisiasa vya MDC, makubaliano yaliyosimamiwa na Rais wa Afrika ya Kusini Thabo Mbeki, mnamo 2009. Inasemekana kwamba, katika kuelekea uchaguzi wa 2018, kuna tetesi kwamba chama cha ZANU-PF, kina mpango wa kumsimamisha tena Robert Mugabe kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho. Baraza la Maaskofu nchini Zimbabwe, linasisitiza serikali, vyombo vya haki na usalama, kila taasisi, kila raia na taifa kwa ujumla, kuhakikisha wanasimamia katiba, wanatetea haki, umoja, amani na utulivu.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiwsahili, Radio Vatican.

 

 

 

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.