2017-06-05 14:35:00

Waconsolata zingatieni: Majadiliano, utu, ndoa, haki na amani duniani


Mashirika ya Wamissionari wa Consolata kuanzia tarehe 22 Mei 2017 hadi tarehe 20 Juni 2017 yanaadhimisha Mkutano mkuu wa Mashirika haya ya kitawa katika hali ya utulivu na amani ya ndani, daima wajumbe wakiwakumbuka na kuwaombea wamissionari wanaotekeleza dhamana na utume wao katika mazingira magumu na hatarishi sehemu mbali mbali za dunia. Mama Kanisa anawahamasisha watawa hawa kuendelea kuwa waaminifu kwa dhamana na utume wa uinjilishaji wa watu, lakini daima wakijitahidi kuboresha karama ya mashirika yao, kwa kupyaisha shughuli za uinjilishaji mintarafu sera na mikakati ya kitume, daima wakiwa makini kusoma alama za nyakati ili kupambana na umaskini mpya unaoendelea kujitokeza duniani!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Mashirika ya Waconsolata, Jumatatu, tarehe 5 Juni 2017, kwa kuwashukuru na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya katika maisha na utume wa Kanisa. Anawataka kuwa na mang’amuzi mazito hali na mazingira ya watu wanaowahudumia  kama sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya uinjilishaji. Anawataka wawe ni mashuhuda na vyombo vya faraja kwa maskini na wanaoteseka Barani Afrika na Amerika ya Kusini! Wawe tayari kuwa ni mashuhuda wa upendo ambao umemiminwa ndani mwao kwa njia ya Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu amewakumbusha wajumbe hawa kwamba, historia ya Mashirika yao kama ilivyo hata kwa familia, inafumbata furaha na majonzi; mwanga na giza; kwani katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kuna baadhi ya wamissionari wa Consolata wamejitosa kwa huduma na kujisadaka kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Sadaka ya maisha yao, iwe ni chachu ya kuendelea kutekeleza dhamana hii kwa ukarimu uliopyaishwa kama kielelezo makini cha utume wao ndani ya Kanisa.

Ili kutekeleza dhamana na utume huu, kuna haja ya kujenga umoja na mshikamano na Mwenyezi Mungu, ili kuambata na kukumbatia huruma na upendo wake, unaopaswa kumwilishwa katika huduma za kimissionari. Huruma na upendo wa Mungu, vipewe kipaumbele cha kwanza kama dhamana na jibu muafaka katika maisha na wito wa kimissionari! Wajenge mazoea ya kuwa karibu na Mwenyezi Mungu, kwa kujitambulisha na Kristo kwa uhuru na mshangao mkubwa kutokana na matendo yake anayotenda kwa ajili ya binadamu.

Hii iwe ni hija ya maisha ya kitawa, kwa kuendelea kugundua siku kwa siku huruma ya Mungu na karama za Yesu ambazo kweli ni utajiri mkubwa kwa maisha ya binadamu; karama zinazopaswa kushuhudiwa kwa njia ya huduma ya kimissionari. Wawe tayari kupokea changamoto za upyaisho wa maisha na utume wao, kwa kuwa karibu zaidi na Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu, ili kutenda kwa ari na moyo mkuu wa kazi ya kimissionari katika maeneo mapya ya uinjilishaji, ambayo wakati mwingine, yanabeba sadaka kubwa kwani yanaonekana kuwa ni changamoto mamboleo. Mwenyeheri Giuseppe Allamano, muasisi wa Mashirika haya, awe ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kuhamasisha shughuli na utume wa kimissionari; kwa kuchachua ari ya kutegemeza Jumuiya za Kikristo zilizowekwa chini ya usimamizi na uongozi wao, hasa zile ambazo zimefunguliwa hivi karibuni.

Shughuli za kimissionari hazina budi kutoa kipaumbele cha pekee katika utamadunisho wa Injili; ushirikiano na mihimili yote ya utume pamoja na kuwa ni watu wa kiasi katika maisha. Wamissionari wa Consolata wawe ni mashuhuda na vyombo vya majadiliano ya kidini; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha, utu na heshima ya binadamu; tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; haki na amani. Baba Mtakatifu anawataka Wamissionari wa Consolata kuendelea kutembea katika matumaini, ili kuwa ni chemchemi inayojenga kwa kububujika kutokana na kukutana na Yesu anayewaenzi na kuwatakatifuza, kwa upendo, faraja, amani na wokovu kwa watu wote. Ni matumaini ya Baba Mtakaatifu Francisko kwamba mwelekeo uliotolewa kwenye Mikutano mikuu ya Mashirika haya mawili itawaongoza kwa ukarimu ili kufuata nyayo za mwanzilishi wao kama zilivyotekelezwa kwa ushuhujaa na ujasiri na watawa wenzao. Mwishoni, amewatakia heri na baraka katika maisha na utume wao, kwa kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Malkia wa utume pamoja na Mwenyeheri Giuseppe Allamano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.