2017-06-02 15:02:00

Papa Francisko awataka watoto kuondoa woga, kuchangia ustawi wa wengi


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 2 Juni 2017 amekutana na kuzungumza na kikundi cha wanafunzi wanaojipatia uzoefu na mang’amuzi ya elimu ya Kikristo maarufu kama “I Cavalieri”, waliomuulizia maswali msingi katika maisha, hususan kuhusu changamoto ya kukubali mabadiliko katika maisha; mchango wa watoto katika kusaidia mchakato wa mabadiliko chanya duniani; Je, ni kwa jinsi gani wanaweza kukabiliana na simanzi pamoja na majonzi ya kuondokewa na wazazi, ndugu na jamaa waliokuwa wanawasaidia na kuwawezesha katika maisha?

Baba Mtakatifu Francisko amewajibu watoto hawa kwa moyo mkuu, upole na unyenyekevu! Amewakumbusha kwamba, maisha ni safari inayoendelea kila siku na hivyo inawapatia nafasi ya kukua na kukomaa katika maisha yao; kwa kukutana na watu wapya kila wakati, jambo ambalo ni changamoto endelevu. Baba Mtakatifu anawataka watoto hawa kutokuwa na woga wa kuacha baadhi ya mambo, ili kuendelea kukua na kukomaa, kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha. Watoto na vijana wawe na ujasiri wa kuvuka kuta zinazoweza kuwakatisha tamaa ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu! Watoto wawe na ujasiri wa kusonga mbele, kwa kuwakumbuka na kuwaheshimu wenzi wao wa safari ya maisha.

Baba Mtakatifu amewahakikishia watoto hawa kwamba, wao wanao mchango mkubwa unaoweza kusaidia kusukuma mbele mchakato wa mabadiliko chanya duniani, licha ya uwezo wao mdogo katika masuala ya elimu, uwezo wa kiuchumi pamoja na nafasi zao katika jamii. Lakini wana uwezo wa kugawana na jirani zao, hata kile kidogo walicho nacho, ili kujenga umoja, udugu na upendo, kwa kuondokana na ubinafsi pamoja na uchoyo, tayari kuwanyooshea wengine mkono wa ukarimu! Wawe na moyo wa upendo. Watoto waanze kujenga utamaduni wa kuwasikiliza na kuwapokea wengine jinsi walivyo! Watoto wanaweza kuleta mabadiliko kwa njia ya ukarimu, udugu, upendo na msamaha wa kweli pasi na kulipizana kisasi. Wajenge moyo wa sala kwa ajili ya marafiki na maadui zao kama anavyofundisha Kristo Yesu kwani Mwenyezi Mungu anawanyeeshea mvua wema na wabaya; warefu kwa wafupi bila ubaguzi.

Baba Mtakatifu anasema, mateso, mahangaiko na machungu wanayokabiliana nayo watoto wadogo, hata wakati mwingine kwa kuondokewa na wazazi, ndugu na jamaa zao waliowapenda, linabaki kuwa ni fumbo ambalo halina jibu la mkato katika maisha ya binadamu. Lakini bado upendo wa Mungu hauna mipaka kwa waja wake. Fumbo la Msalaba ni jibu makini kwa mateso na mahangaiko ya binadamu. Nyuma ya Msalaba, kuna upendo, huruma na msamaha ambao Mwenyezi Mungu anapenda kuwakirimia waja wake. Hata watoto hawa wanapaswa kuanza kufahamu kuhusu fumbo la mateso na mahangaiko ya binadamu, ili kukua na kukomaa katika maisha. Bikira Maria, Mama wa Kanisa anatambua maana ya mateso na mahangaiko ya binadamu, kwani alithubutu kusimama chini ya Msalaba akashuhudia kifo cha Mwanaye mpendwa Yesu Kristo! Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka watoto hawa kuwa na ujasiri, ukarimu, mapendo tayari kusonga mbele na kwamba, katika maisha, wakati mwingine hakuna majibu ya mkato, bali watu hawana budi kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu anayeweza kuwafafanulia maana ya Fumbo la Msalaba katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.