2017-06-02 16:18:00

Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki ni jembe la uekumene duniani!


Maelfu ya Wanachama wa Chama cha Kitume cha Wakarisimatiki Wakatoliki au kama wanavyojulikana na wengine kuwa ni Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki kutoka katika nchi 127, Tanzania ikiwakilishwa na wanachama 120 tayari wamewasili mjini Roma, Italia na wanaendelea na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Uhamsho wa Kikatoliki Duniani. Kilele cha maadhimisho haya ni Siku kuu ya Pentekoste, kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:30 za asubuhi kwa saa za Ulaya. Jumamosi, tarehe 3 Juni 2017 kunafanyika mkesha wa kukata na shoka kwenye Uwanja wa “Circo Massimo” na kuhudhuriwa na Baba Mtakatifu Francisko.

Papa Francisko katika ujumbe wake kwa wanachama wa chama cha Uhamsho wa Kikatoliki anawaambia kwamba, wao kwa hakika ni chombo madhubuti sana cha majadiliano ya kiekumene, yanayoliwezesha Kanisa Katoliki kutembea bega kwa bega na waamini wa Makanisa mengine ya Kikristo; katika utekelezaji wa uekumene wa sala na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wanachama hawa ambao wengi wao wamewasili mjini Roma kuanzia tarehe 31 Mei 2017 wanaendelea na maadhimisho haya kwa: Ibada, makongamano na mikutano mbali mbali pamoja na kutembelea kwenye maeneo ya hija hapa mjini Roma. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa uwepo na utume wao ndani ya Kanisa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Maadhimisho haya yameandaliwa na Chama cha Udugu wa Kikatoliki na Huduma ya Uhamsho wa Kikatoliki Kimataifa. Tukio hili linawashirikisha pia Wakristo kutoka katika Makanisa na Madhehebu mbali mbali, ili kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa karama na mapaji yake kwao!

Baba Mtakatifu anawakumbusha wanachama hawa kwamba kazi ya Roho Mtakatifu ni kuwafundisha na kuwaongoza waamini katika umoja na unaofumbatwa kwenye utofauti. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya uekumene wa sala, huduma, maisha ya kiroho sanjari na uekumene wa damu! Baba Mtakatifu anawahimizwa Wakristo kufanya hija ya pamoja itakayowawezesha wote siku moja waweze kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu! Anawataka kuendelea kuwa waamini kwa amri ya Kristo kwa waja wake, ili wote wawe wamoja kama anavyokaza kusema katika ile Sala ya Kikuhani, maarufu kama “Sala ya Yesu” inayopatikana kwenye Injili ya Yohane sura ya 17.  Yesu mwenyewe ndiye anayeomba umoja kwa Baba yake wa mbinguni kwa ajili ya wafuasi wake, ili kweli ulimwengu uweze kumwamini Kristo aliyetumwa na Baba yake wa mbinguni.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wajumbe wote kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, anatumaini kukutana na kusali pamoja nao kwenye mkesha wa Siku kuu ya Pentekoste, kwenye Uwanja wa “Circo Massimo”. Huu utakuwa ni mkesha wa kiekumene kwa ajili ya Siku kuu ya Pentekoste kwa Mwaka 2017.  Hiki ni kipindi cha sala za kijumuiya, tafakari za pamoja, shuhuda za maisha na utume pamoja na Ibada za Misa Takatifu. Kwa ufupi, hiki ni kipindi cha neema na baraka; Jubilei ni wakati wa kushuruku na kuomba toba na neema ya kuweza kusonga mbele zaidi kwa ari, moyo mkuu, unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani, daima kwa kumwachia Roho Mtakatifu aweze kuwafundisha, kuwakumbusha, kuwaongoza na kuwatakasa na mapungu yao ya kibinadamu, tayari kuambata utakatifu wa maisha!

Wahubiri wakuu wakati wa Mkesha wa Kiekumene, Jumamosi, tarehe 3 Juni 2017 ni Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya Kipapa na Mheshimiwa Giovanni Traettino, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Upatanisho. Baba Mtakatifu Francisko atakapowasili, ataongoza Ibada ya Sala ya Kiekumene, ili kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kulivuvia tena Kanisa lake.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea kukujuza yale yanayojiri katika maadhimisho haya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.