2017-06-01 07:13:00

Mh. Padre Alexander Awi Mello ateuliwa kuwa Katibu mkuu


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre Alexander Awi Mello, kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Alizaliwa tarehe 17 Januari 1971 huko Rio de Janeiro, baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 7 Julai 2001 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre katika Shirika la Mapadre wa Schonstatt. Amekuwa ni Paroko usu kwenye Parokia ya Mama Yetu wa Dores huko Santa Maaria na mratibu wa utume wa vijana Shirika la Mapadre wa Schonstatt huko Brasile na Mkurugenzi wa utume wa vijana kitaifa pia.

Kitaaluma ni mwanataalimungu mahiri aliyejipatia shahada yake ya uzamivu kutoka nchini Ujerumani kunako mwaka 2000 na kwa sasa anahitimisha masomo yake ya Shahada ya uzamivu kuhusu Bikira Maria, kwenye Chuo kikuu cha Dayton, Marekani. Amewahi pia kuwa ni mkufunzi kwenye vyuo mbali mbali vya kipapa ndani na nje ya Brazil tangu mwaka 2000 hadi 2009. Kunako mwaka 2007 amekuwa ni mjumbe wa Sekretarieti ya Mkutano wa Aparecida. Ni mkurugenzi wa Jarida la “Tabor” na amekuwa ni mwandishi mzuri wa makala za katekesi na shughuli za kichungaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.