2017-05-31 12:25:00

Watanzania wanawaombolezea Mzee Ndessamburo na Mzee Francis Kanyasu


Mkongwe wa siasa nchini Tanzania aliyetikisa na kutamba katika siasa ya vyama vingi nchini Tanzania Mzee Pilemon Ndessamburo, aliyewahi kuwa mbunge wa Moshi mjini na Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kilimanjaro amefariki dunia, tarehe 31 Mei 2017. Watanzania wengi watamkumbuka sana kutokana na mchango wake katika maendeleo na medani za siasa za upinzani! Alikuwa ni ngome ya CHADEMA mkoani Kilimanjaro!

Wakati huo huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe leo ametuma ubani na salamu za rambirambi kwa familia ya msanii mkongwe katika fani ya uchoraji Mzee Francis Maige Kanyasu (86), kufuatia kifo cha msanii huyo kilichotokea tarehe 29 Mei, 2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Waziri Mwakyembe ametuma ubani na salamu hizo za rambirambi leo mchana kupitia kwa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa, Godfrey Mngereza, ambaye vilevile amemwelekeza kushirikiana kwa karibu na ndugu na jamaa wa marehemu katika mazishi yake. Katika salamu zake za rambirambi, Waziri Mwakyembe amesema Wizara itahakikisha michango ya wasanii wakongwe kama Mzee Kanyasu, inafuatiliwa kwa karibu na kuwekewa kumbukumbu kwa faida ya vizazi vijavyo. Kufuatia taarifa iliyotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili, hali ya mzee Francis ilibadilika ghafla wakati alipokuwa akipatiwa huduma ya matibabu hospitalini hapo hivyo kupelekea mauti yake. Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.

Imetolewa na

Genofeva Matemu

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo

30/05/2017

 








All the contents on this site are copyrighted ©.