2017-05-28 14:00:00

Vijana wana imani na matumaini kwa Kanisa la Kristo!


Madhabahu ya Bikira Maria Mlinzi ni kati ya madhabahu makuu yaliyoko huko Liguria, Kaskazini mwa Italia kama alivyowahi kusema, Papa Benedikto wa kumi na tano! Hapa ndipo ambapo Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 27 Mei 2017 amekutana na kuzungumza na vijana wa kizazi kipya kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Genova. Kardinali Angelo Bagnasco katika salam zake kwa Baba Mtakatifu amesema, kwamba, vijana waliokuwa mbele yake wamesheheni cheche za furaha na upendo; lakini pia wana shida, mahangiko na changamoto za maisha, ambazo wanataka kumshirikisha Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Bagnasco anasema, vijana wa kizazi kipya wana mwangalia Baba Mtakatifu Francisko kwa jicho la matumaini na uhakika wa usalama wa maisha yao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili kumfuasa Kristo Yesu anayemfahamu na kumwita kila mmoja wao kwa majina yake; wanataka kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kutekeleza mpango kamambe katika maisha yao. Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 inaongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii ni Sinodi inayosheheni furaha na matumaini! Vijana waliokuwa wamekusanyika mbele ya Baba Mtakatifu Francisko walitaka hata wao kuchangia katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, huku wakiwa na ndoto kubwa katika maisha!

Kardinali Bagnasco amemshirikisha Baba Mtakatifu kwamba, mwaka 2016, Jimbo kuu la Genova lilikuwa ni Mwenyeji wa Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, lililongozwa na kauli mbiu “Ekaristi Takatifu chemchemi ya utume.” Tukio hili limekuwa na mafao makubwa kwa vijana wa kizazi kipya Jimbo kuu la Genova kwani, miongoni mwa vijana kumeibuka vijana ambao wanataka kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya kushiriki katika mchakato wa uinjilishaji katika maeneo yao; tayari kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.