2017-05-25 16:16:00

Utakatifu na uzuri wa Sinema viamshe matumaini kwa watu!


Sinema iliyoandaliwa vyema ni katekesi muhimu sana katika utu na heshima ya binadamu. Ni simulizi ya matatizo na changamoto anazokabiliana nazo binadamu, ili kuweza kuibua matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Sinema ina nafasi ya pekee katika maisha ya kijamii, kama sanaa ambayo ni kioo cha jamii kinachoonesha mahangaiko yake ya ndani pasi na kuyapindisha hata kidogo. Sinema pia inamwezesha mtazamaji kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha, kiasi hata cha kugundua uwepo wa Mungu katika hija ya maisha ya mwanadamu.

Huyu ni Mungu anayejifunua katika historia ya mwanadamu kuwa ni mwingi wa huruma na mapendo. Yesu ni uso wa huruma ya Mungu na chemchemi ya matumaini mapya kwa binadamu! Huu ni ushuhuda uliotolewa na Monsinyo Dario Edoardo Vigano’, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican wakati akichangia mada kwenye Tamasha la 70 la Sinema la Cannes, kuhusu: utakatifu na uzuri, Alhamisi, tarehe 25 Mei 2017. Katika kipindi cha miaka 70 iliyopita kumekuwepo na wasanii waliotukuka na kubobea katika fani ya uchezaji wa Sinema waliowaonjesha watu uhalisia wa maisha ya kila siku, kwa kuwakumbusha pia umuhimu wa kujenga mafungamano ya kijamii na huruma.

Hawa ni wasanii ambao wamegusa mambo msingi ya maisha na utu wa mwanadamu yaliyosukumizwa pembezoni; mapambano ya wafanyakazi; urasimu na ukiritimba pamoja na athari zake; huruma na upendo unaobubujika kwa kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengine. Ni wasanii ambao wamejitahidi kuwa ni kioo cha mahangaiko ya wafanyakazi pamoja na tunu msingi za maisha ya kifamilia, zinazowasaidia watu kupyaisha maisha yao! Injili ya matumaini anasema Monsinyo Dario Edoardo Vigano’ ndicho kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 51 ya Upashanaji Habari Duniani, yanayoongozwa na kauli mbiu “Usiogope, maana mimi ni pamoja nawe” kutangaza matumaini na imani katika nyakati hizi”.

Hapa Baba Mtakatifu anawataka wadau wote katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba wanahabarisha kile kilicho kweli kwa uaminifu bila kuwaondolea watu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Huu ni mchango wa mawasiliano ulio wazi na unaojikita katika kipaji cha ubunifu bila kuzama katika ubaya, bali kushuhudia cheche za mambo mazuri zaidi. Ni mwelekeo wa mawasiliano chanya na yanayowawajibisha watu katika mchakato mzima wa upashanaji habari, lengo ni kutoa habari njema zaidi, jambo linalotafutwa pia hata katika Sinema nzuri kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.