2017-05-25 14:55:00

Uinjilishaji wa kina usaidie mchakato wa kukuza na kulikomaza Kanisa!


Majimbo mapya yaliyoundwa hivi karibuni huko Equatorial Guinea yanalenga kupeleka huduma za kichungaji karibu zaidi na familia ya Mungu, changamoto kubwa kwa sasa ni ushirikiano na mshikamano na Askofu mpya ambaye anapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya waamini na Baba wa familia ya Mungu kama anavyokaza kusema, Mtakatifu Agostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa! Hii ni sehemu ya wosia uliotolewa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu Jumatano, tarehe 24 Mei 2017 wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumsimika rasmi Askofu Miguel Angel Nguem Bee wa Jimbo Katoliki Ebebiyin, huko Equatorial Guinea, ambalo lina miaka 35 tangu lilipoanzishwa.

Askofu Nguem Bee mwenye umri wa miaka 47 aliwekwa wakfu tarehe 20 Mei 2017 Jimboni Mongomo na amekumbushwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa kuwa mchungaji mkuu wa Jimbo la Ebebiyin kutokana na uzoefu na mang’amuzi yake katika shughuli za kichungaji, maisha ya kipadre pamoja na majiundo makini ya kiroho na kiutu aliyofanikiwa kuyapata katika hija ya maisha yake hapa duniani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Askofu mpya kwa kushirikiana na mihimili yote ya uinjilishaji, ataweza kusaidia mchakato wa kukua na kukomaa kwa Kanisa mahalia.

Kardinali Fernando Filoni katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee kabisa dhamana na utume wa Kristo Yesu katika mpango wa ukombozi unaowashirikisha waamini wote kuwa ni sehemu ya watoto wapendwa wa Mungu, hali inayowataka kujikita katika utakatifu wa maisha kwa kukuza na kudumisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, daima wakiwa tayari kubadili mtindo wa maisha yao kama ilivyokuwa kwa Paulo Mtume alipokutana na Yesu Kristo Mfufuka akiwa njiani kuelekea Damasko!

Saul aliyekuwa analitesa Kanisa, akageuka na kuwa ni Mwalimu wa Mataifa na chombo cha uinjilishaji, kiasi hata cha kuthubutu kusimama mbele ya wanafalsafa wa Kigiriki na kuwaambia kwamba, kwa hakika: Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kutoka kwa wafu! Na kwamba, hiki ndicho kiini cha Habari Njema ya Wokovu! Wanafalsafa wengi walimbeza na kuwambia kwamba, kwa habari ya ufufuko wa wafu, watamsikiliza siku nyingine tena! Lakini kuna watu waliomsikiliza kwa makini, wakaamini na kubatizwa! Hapa, Mama Kanisa anapenda kuwakumbusha watoto wake kwamba, jambo la msingi ni kujiaminisha kwa nguvu, neema na baraka ya Roho Mtakatifu katika mchakato mzima wa uinjilishaji na kwamba, mafanikio si juhudi za mtu binafsi.

Paulo mtume, alijiaminisha sana kwa Kristo, akashuhudia ukarimu katika uinjilishaji kwa kujisadaka bila ya kujibakiza! Akatangaza Neno la Mungu kwa watu wa mataifa; akawasaidia kuonja wema na ukarimu wa familia ya Mungu kwa njia ya Injili ya upendo. Huu ndio mwaliko unaotolewa kwa Askofu Miguel Angel Nguem Bee wa Jimbo Katoliki la Ebebiyin katika uchanga wake. Waamini wanaalikwa kumtegemea Roho Mtakatifu atakayewafundisha na kuwaongoza katika ukweli wote. Nguvu ya Kanisa inatoka juu na ina uwezo wa kuleta mabadiliko na mageuzi katika maisha ya watu!

Hii ni nguvu inayosimikwa katika msamaha wa Kristo kwa Mtakatifu Petro, ambaye baadaye anathubutu kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia kwamba, Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kutoka kwa wafu! Hiki ni kiini cha imani ya Kikristo! Ndio ujasiri ambao  ulioneshwa pia na Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa mbele ya wanafalsafa wa Kigiriki pale Athene. Kumbe, waamini wanahamasishwa kuwa na ujasiri wa kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza bila kukata wala kujikatia tamaa kwani wanaye Mama Bikira Maria Msaada wa Wakristo. Ni Mama wa Mungu aliyethubutu kusimama chini ya Msalaba na akawa ni Mama wa Kanisa. Alishiriki matukio muhimu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo, akashuhudia Roho Mtakatifu akiwashukia Mitume nao wakatoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka. Nguvu ya Roho Mtakatifu ikae ndani mwao, ili waweze kuwa na ukarimu katika kutangaza na kushuhudia Injili kwa watu wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.