2017-05-25 15:24:00

Twekeni hadi kilindini kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!


Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuonesha ujasiri unaomwilishwa katika ushuhuda wa imani tendaji, kwa kujiaminisha katika uongozi wa Roho Mtakatifu, ili kuweza kufikiri na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Haijalishi ni kiasiĀ  gani cha mafanikio ambacho kiongozi anaweza kufanikisha, lakini jambo la msingi ni kuthubutu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, changamoto ni kuonesha ushirikiano wa dhati na Askofu Miguel Angel Nguem Bee wa Jimbo Katoliki Ebebiyin, huko Equatorial Guinea.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumatano tarehe 24 Mei 2017 alipokutana na kuzungumza na wakleri pamoja na watawa wa Jimbo Katoliki Ebebiyin, huko Equatorial Guinea. Tangu sasa anapaswa kujielekeza zaidi katika shughuli za kichungaji Parokiani kwa kukazia katekesi makini ya awali na endelevu; kwa njia ya huduma ya elimu na afya, ustawi na maendeleo endelevu, ili kusaidia mchakato wa ukombozi wa mtu mzima: kiroho na kimwili. wajielekeze zaidi katika kukuza na kudumisha ari na mwamko wa Kanisa la kimissionari, tayari kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Wakumbuke kwamba, walimwengu mamboleo wanavutwa zaidi na ushuhuda unaomwilishwa katika matendo na kwamba, wamechoka kusikia maneno matupu! Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa; daima wakikumbuka kwamba, Kanisa Barani Afrika linahamasishwa kuwa ni vyombo vya huduma na shuhuda wa upatanisho, haki na amani. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu Barani Afrika kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, kwa kumfuasa kwa uaminifu mkubwa kama kielelezo makini cha utii, ufukara na usafi kamili. Kwa njia hii, kwa hakika watakuwa ni mashuhuda wa upendo wa Kristo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Katika maisha na utume wa Kanisa, kuna matatizo, changamoto na fursa zake, kama viongozi wa Kanisa mahalia, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatweka hadi kilindini katika huduma ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Waamini watambue kwamba, Upadre ni wito na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko: mapadre na watawa wanaweza kuushuhudia umissionari wa Kristo katika utii, ufukara na useja, tayari kuwatangazia watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Ili kufanikisha azma hii, familia ya Mungu nchini Equatorial Guinea, lakini kwa namna ya pekee kabisa Jimbo Katoliki Ebebiyin haina budi kuwa na picha kamili ya Kanisa ambalo wanataka kushiriki kulijenga na kulidumisha kwanza kabisa kama: wakleri, watawa na waamini walei kila mtu kadiri ya wito, dhamana na nafasi yake katika maisha na utume wa Kanisa!

Jambo la msingi ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko, tayari kutoka kifua mbele, ili kuwatangazia na kuwashirikisha wale waliko pembezoni mwa jamii furaha ya Injili, upendo na mshikamano unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyekuwa tajiri, lakini akajishusha, ili kwa njia yake, watu wengi zaidi waweze kutajirika. Huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza! Viongozi wa Kanisa daima wajitahidi kujiaminisha katika nguvu na neema ya Roho Mtakatifu inayotenda hata katika udhaifu na unyonge wao. Wawe ni vyombo vya umoja na mshikamano na maskini; huduma makini kwa watu wote kwa kukazia mambo msingi katika maisha, chemchemi ya furaha ya kweli.

Daima wajifunze kutoka kwa maskini ili waweze kuwa na kiasi pamoja na kushiriki katika mateso na mahangako ya familia ya Mungu, huku wakijitahidi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu! Kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu kwa kuwa na uchu wa mali, bali mali ya dunia na utajiri wake wote utumike kwa ajili ya ujenzi wa ufalme wa Mungu. Matumizi ya rasilimali na utajiri wa Kanisa yajikite katika ukweli na uwazi, uaminifu na uadilifu kwani mambo yote haya yanapaswa kutumika katika mchakato wa Uinjilishaji. Mapadre na Watawa wawe waaminifu kwa mashauri ya Kiinjili kwa kuachana na maisha ya kinafiki na undumila kuwili!

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu anawataka wakleri na watawa kuonesha: utii, ushirikiano na mshikamano na Askofu wao mahalia, kwani uongozi kadiri ya mantiki ya Injili ni huduma kwa familia ya Mungu! Injili itangazwe na kushuhudiwa kwa njia ya mashauri na tunu msingi za maisha ya Kiinjili; kwa kujikita katika ushuhuda unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake na kwamba, Kristo daima ataambatana nao katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa kama alivyofanya kwa wanafunzi wa Emau!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.