2017-05-25 15:54:00

Mapambano ya majanga asilia: Binadamu apewe kipaumbele cha kwanza!


Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kujielekeza zaidi katika mchakato unaopania kuzuia majanga asilia, kutokana na itifaki kuu tatu za utekelezaji zilizotiwa sahihi na Jumuiya ya Kimataifa hivi karibuni. Mwongozo wa Kazi wa Kupunguza Majanga asilia wa Sendai kwa Mwaka 2015 – 2030; Agenda ya Maendeleo Endelevu kwa Mwaka 2030 pamoja na Itifaki ya Makubaliano ya Udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabia nchi wa Paris, 2015. Mwaka 2017 unaonesha umuhimu wa utekelezaji wa itifaki hizi, ili kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, mapambano dhidi ya umaskini, ubaguzi wa kijamii pamoja na kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata mafanikio yanayokusudiwa kuna haja kwanza kabisa ya kujielekeza kwenye mchakato wa kuzuia, elimu na mafunzo yatakayosaidia kupunguza maafa makubwa kwa watu na mali zao pamoja na athari katika mchakato wa ukuaji wa uchumi kwa nchi husika. Jambo la pili ni kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini ambao kimsingi ni waathirika zaidi wa majanga asilia duniani na tatu ni kutambua na kuthamini mchango wa waathirika katika mchakato wa kuzuia, kujibu na kukarabati upya uharibifu unaoweza kujitokeza. Haya ni mambo makuu ambayo yanapewa kipaumbele cha pekee na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika barua yake aliyomwandikia Rais Enrique Pena Nieto, Rais wa Mexico ambaye pia ni Rais wa Jukwaa la Kimataifa Kwa Mwaka 2017 la kupambana na majanga asilia, katika mkutano wao ulioanza tarehe 22 hadi 26 Mei 2017 huko Cancun, nchini Mexico.

Kardinali Parolin anasema, kumekuwepo na maafa makubwa kwa watu na mali zao kutokana na majanga asilia ambayo kimsingi ni matokeo ya utawala mbovu, ukosefu wa mipango sahihi inayosindwa kutoa vipaumbele kwa mfano uvunaji na utunzaji bora wa rasilimali maji ambayo yamekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia. Ikiwa kama maji yataweza kudhibitiwa kikamilifu yanaweza pia kusaidia mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini duniani; ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Kwa maneno machache udhibiti wa majanga asilia umlenge binadamu! Anasema, maskini ni waathirika wakubwa wa majanga asilia duniani kwani hawa ni wale wanaoishi katika mazingira hatarishi zaidi. Kumbe, hawa wanapaswa kuwezeshwa na kushirikishwa katika mapambano dhidi ya maafa asilia. Mbinu hizi zinaweza kuwa ni katika maisha ya kiroho na kimwili, kwani maafa yanapowakumba watu, yanawathiri pia katika maisha yao ya ndani! Mkazo ni ujenzi wa makazi bora kwa waathirika wa majanga asilia.

Waathirika wa majanga asilia wanayo pia mchango katika kuzuia, kutekeleza na ujenzi mpya kwa kuwa na mikakati ya muda mfupi na mrefu katika mapambano dhidi ya majanga asilia. Hapa kuna haja ya kujenga utamaduni wa ushirikishwaji mpana, majadiliano katika ngazi mbali mbali bila kuwasahau watu mahalia, ili kuibua mbinu na mikakati itakayofanyiwa kazi katika ngazi ya chini kabisa hadi kufikia ngazi ya kimataifa. Mwelekeo huu pia unahitaji mabadiliko ya fikra na mfumo wa maisha; kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kifamilia, ili kujenga na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu. Ulaji wa kupindukia ni tatizo kubwa katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Ni matumaini ya Kardinali Parolin kwamba, Jukwaa hili la kimataifa litaweza kulueta mafanikio katika mchakato wa kudhibiti majanga asilia pamoja na kuharakisha maendeleo endelevu kama jibu muafaka wa ushirikiano na udugu kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, Vatican itaendelea kuchangia katika haya kadiri ya uwezo wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.