2017-05-24 15:13:00

Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ni kiini cha imani ya Kikristo!


Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anayemaliza muda wake, Jumatano, tarehe 24 Mei 2017 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ili kusali na kuiombea familia ya Mungu nchini Italia, katika shida, mahangaiko na matumaini yake, kama kielelezo makini cha upendo wa kichungaji unaotolewa sadaka kwa Kristo Yesu hasa wakati huu wanapoadhimisha Mkutano mkuu wa 70 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Katika maisha na utume wao, wanakumbana na changamoto nyingi kama ilivyokuwa kwa Mtume Paulo ambaye anageuziwa kisogo na wanafalsafa wa Athene waliokuwa wanahoji kuhusu “dhana ya ufufuko wa wafu”, kiini cha imani ya Kikristo. Mtakatifu Paulo alitambua umuhimu wa mji wa Athene katika masuala ya kitamaduni na kielimu, lakini akathubutu kuwatangazia na kuwashuhudia: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, daima akiwa waminifu kwa ukweli alioupokea.

Paulo Mtume anamwelezea Mwenyezi Mungu kuwa ni: Muumbaji, chemchemi ya maisha na uhuru wa kweli! Ni Mungu ambaye yuko kati pamoja na watu wake, ili kuwapatia matumaini ya kuweza kusonga mbele licha ya magumu na changamoto za maisha wanazokutana nazo! Anaendelea kufafanua kuhusu historia ya wokovu ambamo Mwenyezi Mungu ni mhusika mkuu anayemkirimia mwanadamu matumaini mapya; anayemjalia mwanga katika mapito yake, ili kamwe asitembee katika giza na uvuli wa mauti!

Kardinali Bagnasco anasema, Mwenyezi Mungu ni muumbaji wa vile vinavyoonekana na visivyoonekana; kazi yote hii inapata utimilifu wake katika Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, katika Fumbo la Umwilisho! Huyu ndiye Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kiini cha imani ya Kanisa, ukawa ni mwanzo wa patashika nguo kuchanika kati ya Paulo Mtume na wanafalsafa wa Athene. Hii ndiyo changamoto endelevu ambayo pia inaweza kujirudia tena na tena katika maisha ya familia ya Mungu nchini Italia.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuwa karibu zaidi na waamini wao; kutweka hadi kilindini katika maisha na utume wa Kanisa; kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu ni Bwana na Mkombozi wa ulimwengu; wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu, kielelezo makini cha imani tendaji! Kanisa linawaalika waamini nchini Italia kuwa kweli ni mashuhuda wa furaha ya Injili katika maisha yao kwa kutambua kwamba, mhusika mkuu katika mchakato wa uinjilishaji mpya ni Roho Mtakatifu atakayewafunulia na kuwafundisha ukweli wote. Waamini wajitahidi kumtambua Kristo Mfufuka kwa njia ya jirani zao na kamwe wasiwe ni watu wenye imani haba “kama kiatu cha raba”!

Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anayemaliza muda wake anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Italia kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, ili aweze kuwakirimia mwanga wa matumani, ili watambue ukweli na wema tayari kufuata na kumshuhudia Mwenyezi Mungu kwa: kupenda, kufikiri na kutenda kama anavyofanya Mungu mwenyewe jambo ambalo kweli linahitaji mwamini kujiaminisha mbele ya Mungu ili aweze kutenda kadiri anavyotaka Mungu mwenyewe. Waamini wajichotee mwanga wa upendo na huduma kutoka kwa Kristo Yesu. Mwishoni, Kardinali Bangasco ametumia fursa hii kuwashukuru Maaskofu wenzake waliompatia dhamana ya kuongoza Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa kipindi cha miaka 10. Kwa kipindi chote hiki, amepata nafasi ya kukutana na Maaskofu wote, changamoto ni kuendelea kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu nchini Italia sanjari na kuendelea kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro ambaye ana uhusiano wa pekee na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.